Makala

BLACK & WHITE: Namba hazidanganyi, Okwi jiadhibu kabla hujaadhibiwa

on

BARUA YA WAZI KWA EMMANUEL OKWI

KWAKO ‘Mfalme’ Emmanuel Okwi, natumai umzima wa afya tele, hapa Bongo umetukuta tuko salama na hatuna mpya zaidi ya suala la Azam FC kutwaa ubingwa wa kombe la Mapinduzi. Wametwaa kwavile walilihitaji mno wakaenda na kikosi kamili, sio kama watoto wa Kariakoo walioenda ‘vipande vipande’.

Na wewe sikukuona kule ‘Zenji’ ingawa sikustaajabu sana kwavile najua miaka yote likizo yako huanza kabla ya Christmas (kumbukumbu ya siku yako ya kuzaliwa) na kumalizika wiki moja ama mbili baada ya mwaka mpya. Hiyo ni bila kujali timu yako inakabiliana na michuano gani, hatari sana.

Mara kadhaa (miaka ya nyuma) uliwahi kwenda Uganda na ukachelewa kurejea kwa sababu nyepesi zinazofanana na hizi zilizotolewa safari hii (majeruhi au mapumziko). Nikuambie tu huku nyuma huwa wanakusema sana, wanakulalamikia sana, tatizo ni kwamba unafahamu vizuri udhaifu wao, ukirudi unapiga kazi ya ‘maana’ wanasahau kila kitu ndio sababu husikii malalamiko yao.

Najua hiyo Januari 18 katika mchezo wenu dhidi ya Singida United ndio siku yako ya kuwasahaulisha ‘shida’ zao. Hiyo ni hata kama ungetua nchini Januari 17, bado una uwezo wa kutisha, kwani ukiamua lako huwa unashindwa wewe?.

Najua mambo mengi sana kuhusu wewe, najua ukubwa wa kipaji chako, najua umahiri wako, najua unavyojitoa kwa asilimia 100 ukiwa uwanjani. Najua unavyopendwa na wanasimba lakini cha kufurahisha zaidi najua wewe ndio mchezaji msumbufu kuliko wote Tanzania.

Ngoja nikukumbushe jambo moja halafu baada ya hapo ufanye tafakuri ya kina. Tangu timu yako ya Simba iliyokusajili kwa kiasi cha dola 50,000 (zaidi ya Sh 100 milioni), itue hapa nchini ikitokea Afrika Kusini ilikoweka kambi ya maandalizi msimu mpya wa ligi, imeshacheza jumla ya mechi 22.

Simba imecheza mechi moja ya Simba Day, moja ya Ngao ya Hisani, 12 za ligi kuu, nne za Kombe la Mapinduzi na nne za kirafiki. Katika mechi hizo wewe umecheza tisa tu ambazo ni sawa na asilimia 40 pekee ya mechi zote. Namba hazidanganyi, hapa umefeli ‘mwanangu’.

Mchezaji muhimu kama wewe ukiwa bila majeraha makubwa kucheza mechi chini ya asilimia 50 ni kutoitendea haki klabu yako, narudia tena umefeli vibaya mno na usisubiri kuadhibiwa, jiadhibu mwenyewe ndani ya nafsi yako.

Naamini Simba chini ya uongozi makini wa kaimu Rais Salim Abdallah ‘Try Again’ hauwezi kulikalia kimya jambo hili, watafanya tu jambo hata pachelewe lakini ni busara wewe mwenyewe ukatathmini mchango wako katika timu halafu ukafanya maamuzi moyoni mwako. Usisahau wewe ni mchezaji wa kimataifa.

Kukosa mechi tano kati ya 12 za ligi kuu ni tatizo kubwa, kutocheza hata mechi moja ya kirafiki huku ukikosa moja ya kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) na nne za kombe la Mapinduzi ni kutoonyesha thamani yako halisi klabuni hapo. Usisahau kutafakari haraka ili uchukue hatua.

Mwisho wa barua yangu nikuambie jambo moja, ili ndoto zako za kucheza Ulaya kwa mafanikio zitimie unahitajika kuacha tabia ya hii ya usumbufu, kama unavyowajibika kwa asilimia 100 kwenye mechi basi unapaswa pia kuwajibika hivyo hivyo kwa kushiriki mazoezi na wachezaji wenzako katika vipindi vyote.

Uwe na siku njema.

Mimi Karim Boimanda

Mzee wa Black & White

0788334467

 

Tafadhali bonyeza picha hii hapa chini ku’Subscribe kwenye chaneli yetu ya BOIPLUS TV (YouTube)

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU KWA HABARI ZAIDI
Washirikishe rafiki zako habari hii kwa kuwatumia kupitia mitandao ya kijamii hapa chini

About Karim Boimanda

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *