Makala

BLACK & WHITE: Sababu za Okwi, Mavugo, Niyonzima kutoonekana uwanjani

on

SIMBA ilifanya usajili wa ‘kutisha’ mwanzoni mwa msimu huu wa ligi kwa kujumuisha majina kadhaa makubwa kwenye orodha hiyo. Usajili huo uliwatisha sana wapinzani huku ukileta furaha na matumaini tele kwa Wanamsimbazi.

Hadi sasa huwezi kusema Simba hawajanufaika na usajili huo ila kutokana na matarajio makubwa mno waliyokuwanayo mashabiki wa timu hiyo, imepelekea wahisi kwamba bado kiwango hakiendani na uzito wa kikosi chao.

Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 26 huku pia ikitoa kinara wa mabao, Emmanuel Okwi aliyetupia mabao nane. Hiyo ni ishara kuwa mambo si mabaya. Sasa wekundu hao wa Msimbazi wapo kwenye kombe la Mapinduzi mjini Zanzibar baada kutolewa katika hatua ya pili katika kombe la shirikisho (ASFC) jambo ambalo limeongeza chumvi kwenye mawazo ya mashabiki hao.

Katika kombe la Mapinduzi visiwa Zanzibar Simba imeanza kwa sare ya bao moja dhidi ya Mwenge ikiwa bila nyota wake Okwi, Haruna Niyonzima, Laudit Mavugo na usajili mpya, Asante Kwasi. Jambo hili limesababisha wadau wengi wahoji sababu za kukosekana kwao na ndipo BOIPLUS ilipoamua kukusanya taarifa za nyota hao.

EMMANUEL OKWI
‘Mfalme’ anayejijua anapendwa Simba, utawaambia nini mashabiki wa timu hiyo kwa Okwi?. Straika huyu amekuwa akiwakwaza Simba kwa tabia yake ya kuchelewa kurejea nchini kila anapoondoka kwenda kwao Uganda, lakini mara zote mambo yake ya uwanjani yamekuwa yakiwasahaulisha kila kitu.

Taarifa za awali zilidai kwamba Okwi alipata maumivu ya ‘enka’ hivyo asingeweza kutumika ndipo aliporuhusiwa kurudi nchini kwao Uganda.

Baada ya muda mrefu kupita bila kurejea huku wadau wakihoji kwanini ‘mgonjwa’ Okwi akajiuguze kwao wakati Niyonzima anaugulia kambini ndipo msemaji wa klabu hiyo Haji Manara aliponukuliwa akisema nyota huyo alipewa ruhusa ambayo ilimalizika juzi Januari 2 huku akisisitiza ataingia nchini muda wowote.

Yanapokosekana majibu watu hutafuta majibu, asubuhi ya leo kumekuwa na mijadala mikubwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya baadhi ya magazeti kuripoti kuwa Okwi yupo kwenye mgomo baridi akishinikiza kulipwa madai yake ya pesa za usajili.

BOIPLUS iliamua kufuatilia jambo hili ndipo mtu wa karibu wa Mohamed Dewji ‘Mo’ ambaye alifanikisha usajili wa nyota huyo alipofunguka kuwa ‘Mfalme’ huyo wa Msimbazi hadai hata senti moja ya usajili.

“Huyo ni katika wachezaji ambao walipewa pesa zote mara baada ya kukamilisha usajili wao, hadai kitu labda kama kuna tatizo jingine,” kilisema chanzo chetu hicho.

Black & White
Kuna maswali kadhaa ya kujiuliza kabla hatujafika kwenye hatma, kama Okwi aliumia kwanini akajiuguze kwao?, kama alipewa ruhusa hadi Januari 2 kwanini hadi leo Januari 4 hajaripoti kambini akijua timu ipo kwenye mashindano?.

Ni wazi kuwa hapa kuna tatizo, kama shida si madai basi Okwi ni yule yule wa mwaka jana na juzi. Okwi anayeamini kuwa hata awaudhi vipi wanasimba, akija tu miguu yake itawasahaulisha kila kitu.

Laudit Mavugo

LAUDIT MAVUGO
Hakuwa kwenye wakati mzuri tangu kuanza kwa msimu huu akitupia mabao mawili tu hadi sasa timu yake ikiwa imeshuka dimbani mara 12 kwenye ligi kuu. Tatizo la kwanza likiwa ni kupata dakika chache uwanjani lakini hata pale anapoanza amekuwa akionyesha kiwango duni.

Baada ya kutoka kwenye michuano ya Chalenji akiwa na kikosi cha Burundi, Mavugo alikuwa tayari kurudi kujiunga na Simba lakini kocha Masoud Djuma akamwambia “Relax, nenda nyumbani kapumzike hadi nitakapokuhitaji.”

Kwa mujibu wa kocha huyo, aliamua kumpa mapumziko hayo ili ajiweke sawa kisaikolojia kabla ya kurejea na kuanza kupigania namba kikosini hapo. Hata hivyo, jina la Mavugo limeonekana kwenye orodha ya wachezaji walio katika kikosi cha Simba kitakachoshuka kumenyana na Jamhuri usiku wa leo.

Haruna Niyonzima

HARUNA NIYONZIMA
Kiungo huyu raia wa Rwanda mwenye ‘udambwi’ mwingi hajaonekana uwanjani kwa muda mrefu kutokana na majeraha yanayomsumbua.

Yupo kambini na timu mjini Zanzibar akifanya mazoezi na wenzake lakini ni wazi afya yake haijaimarika ndio sababu kocha amesema hajaanza kumtumia kama ilivyo kwa Shomari Kapombe.

Asante Kwasi

ASANTE KWASI
Usajili wa beki huyu uliwapa wanasimba faraja kubwa wakiamini ataziba vilivyo pengo la Method Mwanjali aliyeondoka. Kwasi yupo Zanzibar na katika mchezo wa kwanza mtandao rasmi wa klabu hiyo ulimtaja katika orodha ya wachezaji 11 ambao wangeanza katika mechi hiyo.

Cha kushangaza na kilichozua maswali mengi ni kitendo cha yeye kuonekana jukwaani wakati mchezo huo ukiwa unaenda kuanza. Hata hivyo, kocha Masoud amewatoa hofu wanasimba kwa kusema “ni mambo ya kiufundi tu, ila itafika siku ataanza kumtumia”

Simba itashuka dimbani saa 2:15 usiku wa leo kupepetana na Jamhuri waliobutuliwa mabao 4-0 na Azam jioni ya jana. Kwasi yumo katika kikosi kitakachoanza.

 

Bonyeza picha hii hapa chini ili ku‘SUBSCRIBE kwenye chaneli yetu ya YouTube kwa jina la BOIPLUS TV;

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU KWA HABARI ZAIDI
Washirikishe rafiki zako habari hii kwa kuwatumia kupitia mitandao ya kijamii hapa chini

About Karim Boimanda

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *