Kitaifa

KIMAHESABU: Huyu ndiye mbabe Azam vs Yanga

on

MASAA 26 yamesalia kabla wababe Azam FC hawajawakaribisha mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Vodacom, Yanga kwenye dimba la Azam Complex huko Chamazi jijini Dar es Salaam katika mchezo wa ligi kuu uliovuta hisia za watu wengi.

Azam ipo pointi mbili tu nyuma ya vinara Simba wenye pointi 32 huku Yanga wenyewe wakikamata nafasi ya tatu baada ya kujizolea pointi 25. Azam wameipania mechi hiyo ili waendelee kuwa kwenye nafasi za juu wakati inamaliza mzunguko wa kwanza.

Yanga kwa upande wao wanafanya maandalizi ya nguvu ili kuibuka na ushindi katika mechi hiyo matokeo yatakayowasaidia kupunguza ‘gap’ kati yao na timu hizo mbili zilizo juu yao. Mtandao wa BOIPLUS umekusanya takwimu za timu hizo ili kujua nani ni mbabe wa mwenzake.

Azam na Yanga zimekuwa na matokeo yasiyotabirika na yanayobadilika kila mara wanapokutana huku kwa upande wa ligi kuu timu hizo zikiwa zimeshakutana mara 18 tangu walipocheza mechi yao ya kwanza Oktoba 15, 2008 ambapo Yanga iliibamiza Azam mabao 3-1.

Katika mechi hizo Yanga wameonekana kuwa wababe kwa kuwafunga Azam mara sita huku Wanalambalamba hao wakiibuka na ushindi mara tano na mechi saba zikimalizika kwa sare. Jumla ya mabao 26 yalifungwa katika michezo hizo 18 ikiwa ni wastani wa bao moja kila baada ya dakika 62.

Timu hizo pia zimeshawahi kukutana mara mbili kwenye kombe la Kagame ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika fainali ya 2012 huku Azam wenyewe wakilipa kisasi 2015 pale walipoibamiza kwa penati 5-3 hatua ya robo fainali kabla hawajatwaa kombe hilo.

Katika michuano ya kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) timu hizo zimekutana mara moja tu ikiwa ni katika fainali ya 2016 pale Azam walipokubali unyonge kwa kupokea kipigo cha mabao 3-1 kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.

Baada ya Simba SC kupotea kwenye ramani za ubingwa, timu za Yanga na Azam zilihodhi nafasi ya kwanza na ya pili hivyo kufanikiwa kucheza mechi za Ngao ya Hisani kwa misimu minne mfululizo kuanzia 2013 hadi 2016.

Katika mechi hizo nne Azam walifanikiwa kushinda mara moja tu 2016 pale walipoibamiza Yanga kwa penati 4-1 lakini kabla ya hapo watoto wa Jangwani ‘waliikodi’ ngao hiyo wakitwaa mara tatu mfululizo kwa kuipa Azam vipigo vya 1-0 (2013), 3-0 (2014) na penati 8-7 (2015).

Mashindano ambayo Yanga wamekuwa wanyonge sana kwa Azam ni Kombe la Mapinduzi ambapo hadi sasa wamekutana mara tatu, 2012 Azam walishinda mabao 3-0, 2016 mechi yao ikamalizika kwa sare ya bao moja lakini mwaka jana Azam wakafanya mauaji kwa kuifunga Yanga mabao 4-0.

Timu hizo ambazo kila moja imejinasibu kuibuka na ushindi katika mechi ya kesho itakayochezeshwa na Israel Nkongo, zimekutana mara mbili tu katika mechi zisizo za kimashindano (kirafiki) ambapo Disemba 18, 2010 Azam waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 huku wakiibamiza tena mabao 2-0 Disemba 20, 2011 kwa mabao ya Mrisho Ngassa na Gaudence Mwaikimba.

Kwa ujumla timu hizo zimekutana mara 29, Yanga wakiwa wababe kwa kushinda mara 11 na Azam wakiibuka kidedea mara 10 wakitoka sare katika mechi nane. Takwimu hizi zinaonyesha kihistoria Yanga wameizidi kete Azam, je, wataitumia mechi hii kuendeleza ubabe wao au Azam watasawazisha na kufanya kila moja iwe imeshinda mara 11?.

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU KWA HABARI ZAIDI
Washirikishe rafiki zako habari hii kwa kuwatumia kupitia mitandao ya kijamii hapa chini

About Karim Boimanda

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *