Afrika

Kipa Kenya afunguka ‘uchawi’ wa kudaka penati tatu

on

KIPA wa timu ya Taifa ya Kenya, Matasi Patrick ameweka wazi jambo lililomfanya adake penati tatu kati ya tano alizopigiwa katika fainali ya kombe la Chalenji iliyoshuhudiwa Kenya ikitwaa ubingwa kwa kuifunga Zanzibar kwa mikwaju ya penati 3-2.

Matasi ambaye alikuwa nyota wa mchezo huo aliiambia Azam TV kuwa amedaka penati hizo baada ya kufuata maelekezo ya kocha wake aliyemwambia asithubutu kuchezacheza wakati mpinzani akijiandaa kupiga penati.

“Kocha aliniambia nitulie kabisa, nisichezecheze wala nisifanye chochote hadi mpira upigwe. Jambo hilo pamoja na kucheza kitimu yametusaidia kutwaa ubingwa huu.” Alisema Matasi.

Wachezaji wa Harambee Stars wakishangilia na kombe lao

Timu hizo zililazimika kuingia katika muda wa nyongeza baada ya dakika 90 kumalizika zikiwa zimefungana bao 1-1 yaliyofungwa na Ochieng Ovella dakika ya tano kabla Khamis Musa hajaisawazishia Zanzibar dakika 87.

Katika muda wa nyongeza Kenya walitangulia tena kupata bao dakika 97 lililofungwa na Choka Masoud aliyeingia badala ya Ovella lakini dakika mbili baadae Khamis aliisawazishia tena Zanzibar na kufanya dakika 120 ziishe timu zikiwa sare ya mabao mawili.

Katika hatua ya matuta ndipo Matasi alipoibuka shujaa baada ya kupangua penati tatu za Zanzibar hali iliyomfanya aondoke na tuzo mbili ambazo ni ya Kipa Bora pamoja na Mchezaji Bora wa michuano hiyo huku mkenya Derick Nsibambi akitwaa kiatu cha dhahabu baada ya kutupia mabao manne.

Matasi alipangua penati za Adeyum Saleh, Khamis na Mohamed Issa huku za Feisal Abdallah na Mudathir Yahaya zikitinga nyavuni. Kwa upande wa Kenya Jockins Atudo, Weslay Onguso na Samuel Onyango walikwamisha nyavuni wakati Dancun Otieno penati yake ikidakwa.

Mabingwa Kenya wamepewa zawadi ya kombe, medali na dola 30,000 (zaidi ya sh 60 milioni) huku Gavana wa Kaunti ya Machakos akiwazawadia sh milioni moja za Kenya (sh 20 milioni) sawa na aliyotoa makamu wa Rais, Wiliam Ruto.

Zanzibar waliokamata nafasi ya pili wamelamba medali na dola 20,000 huku mshindi wa tatu Uganda wakivishwa medali na dola 10,000.

 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU KWA HABARI ZAIDI

About Karim Boimanda

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *