Makala

Mapinduzi Cup ilivyomaliza siku 725 za Kessy bila bao Yanga

on

ILIKUWA Juni 20, 2016 siku ambayo Yanga walifanikiwa kukamata saini ya mlinzi wa kulia (aliyekuwa akiitumikia Simba wakati huo), Hassan Ramadhan Kessy na kumvisha jezi yenye rangi za kijani na njano akiachana rasmi na zile nyekundu na nyeupe.

Baada ya usajili wake kukumbwa na sintofahamu kadhaa hasa baada ya Simba kulalamika kuwa Yanga walimsainisha akiwa na mkataba nao, vigogo hao walimalizana kwa usimamizi wa Shirikisho la Kandanda (TFF) na nyota huyo kuanza rasmi kuwatumikia watoto wa Jangwani.

Mara baada ya kujiunga na Yanga, Kessy alionekana kuwa mchezaji mwenye kujituma sana huku akipambana vikali kupata namba ya kudumu kikosini hapo ila akakutana na wakati mgumu kumuondoa Juma Abdul ambaye alikuwa ametoka kushinda tuzo ya mchezaji bora wa ligi kuu ya Vodacom 2015/16.

Hata hivyo mwishoni mwa msimu uliopita beki huyo alipata nafasi katika mechi tano za mwisho zilizoipa ubingwa Yanga ambapo alionyesha uwezo mkubwa uliowafanya wanayanga waone sababu kuu ya usajili wake kikosini hapo.

Kessy (katikati) akiwa na Juma Abdul (kulia)

Tofauti na mabeki wengine wa pembeni, Kessy alikuwa hajawahi kuifungia timu hiyo bao lolote tangu asajiliwe hadi Januari 4 alipofunga bao la ushindi dhidi ya JKU kwenye mechi ya hatua ya makundi ya michuano ya kombe la Mapinduzi inayoendelea visiwani Zanzibar.

Hizo ni sawa na takribani siku 725 alizoitumikia Yanga ukiwa ni muda ni mrefu sana kwa mabeki wa pembeni wa kiwango chake kukaa bila kufumania nyavu. Kessy ameileza BOIPLUS nini hasa tatizo la ukame huo licha ya kucheza katika eneo linalomruhusu kupanda na kushambulia.

“Jukumu la kwanza la beki wa pembeni ni kuzuia ndipo linafuata hilo la kushambulia, mimi nimechagua kutimiza kwanza jukumu langu la msingi kwa asilimia mia, baada ya hapo mazingira yakiruhusu napanda kama hayaruhusu nazuia tu.

“Tatizo ni hofu ya kukosea, unadhani vile nilivyojilipua kupanda kama tungepoteza mpira tukashambuliwa na kufungwa watu wangenielewa?, nawashauri mabeki wenzangu pia wakati mwingine wasiogope kukosea, wapige moyo konde na kupanda ila wawe makini,” alisema Kessy.

Beki huyo mzaliwa wa Morogoro alisema yeye ana uwezo mkubwa sana wa kupandisha mashambulizi na akiamua atakuwa anafunga mabao mengi tu ila siku zote anaangalia aina ya mpinzani wanayepambana nae.

“Kwenye mechi ile na JKU dakika zilikuwa zimekwisha, sikuona cha kupoteza ndio sababu nilikaa kule nyuma nikajisemea moyoni ‘ngoja nipite nikafunge’, hapo niliondoa kabisa mawazo ya sisi kufungwa, ila isingekuwa rahisi kufanya vile kwa dakika za mwanzo,” alimaliza.

Kuhusu ushindani wa namba Kessy alisema huu ni mwaka mpya na yeye amekuja upya, ikitokea akapewa nafasi hatoipoteza na kocha atakuwa akimpa nafasi kila mara.

Yanga wametolewa na URA katika michuano hiyo kwenye hatua ya nusu fainali kwa mikwaju ya penati 5-4 hapo jana.

Tafadhali bonyeza picha hii hapa chini ku’SUBSCRIBE kwenye chaneli yetu ya YouTube kwa jina la BOIPLUS TV

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU KWA HABARI ZAIDI
Washirikishe rafiki zako habari hii kwa kuwatumia kupitia mitandao ya kijamii hapa chini

About Karim Boimanda

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *