Makala

MKEKA WANGU: Timu mbili tu ndio zitalingana pointi kileleni wikiendi hii

on

HABARI ndio hiyo……. Jumapili jioni chungulia msimamo wa ligi kuu ya Vodacom utaelewa vema ninachomaanisha. Huu sasa ndio mwanzo wa kila ‘mtu’ kurudi kwenye makazi yake ya kudumu. Ile habari ya kila wikiendi basi timu tatu hadi nne zina idadi sawa ya pointi kileleni imefikia tamati.

Hapa leo mzee wa MKEKA WANGU natumia namba na utabiri kuimarisha hoja yangu. Najua kuna wakati utabiri huwa unachana ‘mikeka’ ya watu lakini wazungu wanasema “numbers don’t lie”, kwahiyo naamini baada ya wikiendi nitaibuka mshindi katika hili.

Msimamo wa ligi unaonesha timu za Simba, Mtibwa, Yanga na Azam zina pointi 16 kila moja huku Simba ikikaa kileleni kwa ‘kitonga’ cha tofauti kubwa ya mabao ya kufunga na kufungwa. Timu hizi zote zina mechi ngumu wikiendi hii, hizi ndizo zitakazotumika kuzipanga upya kulingana na ubora.

 

Ndanda FC vs Mtibwa Sugar

Timu hizi zinafanana sifa mbili, zote zina washambuliaji butu lakini wana safu nzuri za ulinzi. Nisipoweka sare hapa ni sawa na kupiga teke kapu la pesa za ‘Mhindi’, hakuna namna, hii ‘game’ itaisha kwa sare ya bila mabao.

Katika mechi nane ambazo Ndanda imecheza, ni timu moja tu(Lipuli) ndio imeifunga mabao zaidi ya moja walipoibuka na ushindi wa mabao 2-1. Lakini pia Kagera Sugar ndio pekee wamefanikiwa kuifunga Ndanda zaidi ya bao moja walipoichapa 2-1.

Mtibwa wenyewe wamewahi kupata ushindi wa 2-1 mara moja tu dhidi ya Mbao FC huku wenyewe wakiwa hawajawahi kufungwa zaidi ya bao moja wakitoka pia sare tasa mara mbili, dhidi ya Yanga na pia Singida United.

 

Mbeya City vs Simba

Bonge la mechi hii, tangu siku ya kwanza Mbeya City inakutana na Simba hakujawahi kuwa na mechi ndogo baina yao bila kujali inachezwa uwanja gani. Mara zote matokeo ya mwisho yamekuwa  yakibaki kuwa matokeo tu na wala hayajawahi kutoa taswira ya mechi yenyewe ilivyokuwa.

Hata hivyo siwezi kuacha ku’bet hapa eti kwavile mechi ya hawa jamaa imekuwa haieleweki, mkeka si utakuwa haujakamilika bwana. Simba itaibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City hiyo Jumapili na itaendelea kukaa kileleni.

 

Azam FC vs Ruvu Shooting

Hapa hakuna ‘story’, Azam wanaizidi kwa mbali sana Ruvu Shooting katika nidhamu ya mchezo, mnaweza kupiga kelele kuwa wanapaki basi na mpira wao hauvutii, lakini huo ndio mfumo wa mwalimu Aristica Cioaba.

Muda mwingi wanakuwa katika eneo lao kwa umakini mkubwa huku wakiwategemea makinda wao wanaoongozwa na Mbaraka Yusuf katika kufanya mashambulizi ya ghafla ambayo nina uhakika Ruvu Shooting hawataweza kuyazuia yote.

Mwisho wa mchezo huu Azam 2, Ruvu 0. Tuonane hapa kesho jioni baada ya mechi zote ushuhudie mkeka wangu utakavyokuwa ume’tick.

 

Singida United vs Yanga

Ni vita ya wataalam George Lwandamina na Hans van der Pluijm, hakuna mwingine wa kuamua mechi hii zaidi ya wao, nimewachungulia nimeona game hii inaisha kwa sare ya bao moja.

Singida wana kikosi imara kilichosheheni vipaji, wana mwalimu ‘mtundu’ wa mbinu anayeijua vizuri Yanga, lakini tabia yao ya kushambulia kwa ‘mihemko’ itawafanya washindwe kuwazuia Yanga wasipate bao leo.

Mabeki wa pembeni wa Singida wana uwezo mkubwa wa kupandisha mashambulizi huku wakilinda, lakini kuna dakika watasahau kuwa Yanga ndio timu inayosifika kwa kuibua mawinga wakali, hapo ndipo sare inapopatikana.

Kwa matokeo haya inamaanisha Simba na Azam ndio timu pekee zilizo kileleni zitafanikiwa kupata pointi tatu wikiendi hii, hivyo kumaanisha kuwa zitafungana pointi kila moja ikiwa na 19 huku Mtibwa na Yanga zikiwa na pointi 17 kesho jioni.

Niwekee mkeka wako kwenye comment hapa chini.

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU KWA HABARI ZAIDI
Washirikishe rafiki zako habari hii kwa kuwatumia kupitia mitandao ya kijamii hapa chini

About Karim Boimanda

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *