Burudani

+VIDEO: Mr. Nice kumshtaki Young Dee kisa kuibiwa King’asti yake

on

MWANAMUZIKI mkongwe wa muziki wa kizazi kipya maarufu kama Bongo Flava, Lukas Mkenda ‘Mr. Nice’ amepanga kumshtaki rapa chipukizi Young Dee kwa alichokiita kuwa ni wizi wa kazi yake aliyoifanya miaka mingi iliyopita.

Mr. Nice amemlalamikia Young Dee kwa kunakili mtindo na maneno yaliyomo kwenye wimbo wake uliotamba sana miaka hiyo ‘King’asti’ ambapo kinda huyo ameweka kwenye wimbo wake mpya uitwao ‘Kiben10’.

Akizungumza katika mahojiano kwa njia ya simu na BOIPLUS, Mr. Nice ambaye anaishi nchini Kenya alisema hamfahamu Young Dee na hajawahi kumruhusu mtu yeyote kuurudia wimbo huo huku akiahidi kumshtaki.

“Nimeusikia huo wimbo, huyo Young Dee mimi simfahamu na sijawahi kukutana naye, sijamruhusu mtu yeyote yule kufanyia remix nyimbo zangu.

“Huyo anayejiita Young Dee kama yeye ni msanii anatambua kabisa mambo ya hati miliki, hivyo anastahili adhabu mara mbili, na mimi nakamilisha taratibu, nitasimamia suala hili kuhakikisha nakomesha tabia hii,” alisema Mr. Nice kwa hasira.

Hili ni sakata la pili kwa siku za hivi karibuni baada ya kushuhudia bendi ya Msondo Ngoma ilivyouandikia barua uongozi wa kundi la muziki la WCB linalomilikiwa na msanii Diamond Platnumz kutaka walipwe sh 300 milioni kwa kutumia ‘melody’ yao ya ala ya saxaphone katika wimbo wao wa ‘Zilipendwa’.

Hata hivyo hakuna taarifa rasmi zinazoeleza kama wakongwe hao wamelipwa madai yao au sakata hilo lilimalizwa kimya kimya.

Tazama video hii hapa chini ufahamu zaidi alichozungumza Mr. Nice.

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU KWA HABARI ZAIDI
Washirikishe rafiki zako habari hii kwa kuwatumia kupitia mitandao ya kijamii hapa chini

About Boiplus Media

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *