Makala

Pawasa aibuka na kuwachana viongozi, wachezaji Simba

on

MCHEZAJI wa zamani wa Simba na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stas’, Boniface Pawasa amevunja ukimya na kuwatolea ‘povu’ wachezaji na viongozi kutokana na matokeo mabovu ya timu hiyo.

Pawasa mchezaji aliyefanya vema na kikosi hicho enzi zake, aliamua kufunga vitu ambavyo viongozi pamoja na wachezaji wanapaswa kufanya endapo watahitaji kufanya vyema kwenye michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika.

HAKUNA MAFANIKIO BILA NIDHAMU NA KUJITAMBUA KWA WACHEZAJI
Pawasa anabainisha kuwa endapo Simba itahitaji kufanya vema katika michuano yoyote ile kuanzia Ligi Kuu na michuano ya kimataifa ni lazima wachezaji wajitambue na wawe na wito.

Anasema ndani ya Simba wachezaji wamekosa nidhamu kabisa na kujituma akitolea mfano tukio la jana baada ya Shiza Kichuya kufanyiwa mabadiliko na kuamua kwenda kukaa jukwaani kuwa ni utovu wa nidhamu uliopitiliza.

“Simba ilikuwa na wachezaji kama akina Selemani Matola, Mohamed Mwameja akina Pawasa leo hawapo kuna wengine, sasa huyo Kichuya anatolewa analaumu yeye ni nani, japokuwa ni mchezaji mzuri asijione ni mkubwa kuliko Simba, hata Messi na Ronaldo wanatolewa uwanjani sembuse yeye,” alisema Pawasa.

Kichuya akiwa jukwaani baada ya kutolewa uwanjani

Hata hivyo kocha Masoud Djuma aliiambia BOIPLUS kuwa yeye ndiye aliwaruhusu Kichuya na Jonas Mkude kutokaa benchi na badala yake waende wakafanyiwe ‘massage’ ndani

SIMBA ITATISHA TU AFRIKA
Kuelekea michuano ya kimataifa Pawasa amesema kikosi chao kina uwezo mkubwa wa kufanya vizuri katika mashindano hayo endapo wachezaji na viongozi wakitekeleza majukumu yao ipasavyo kwani wana kikosi kizuri.

“Sina mashaka kabisa na Simba kuelekea michuano ya kimataifa, mfano halisi mechi ya jana japo walipoteza mchezo ila timu ilicheza vizuri na kuonesha kujengeka zaidi.

“Naona mwalimu kaleta mfumo mpya ambao unaendelea kuzoeleka, mfano hali jana Kwasi, Nyoni na Juuko walielewana sana sema ndio hivyo mwisho wa siku mpira ni mabao,”.

USIMPIMIE KOCHA DJUMA
Pawasa anasema, anatambua Djuma ni kocha asiyependa mzaha hata kidogo toka akiwa kiungo mkabaji wa APR hadi sasa ni kocha akimtaja kuwa ni mtu mwenye misimamo mikali.

“Djuma ni kocha mwenye misimamo na hapendi ujinga kabisa, ninachokiona aongozewe nguvu na mwenzake ambaye watamleta aendane nae, tena ikiwezekana wamuache amchague anayemuhitaji yeye ili waweze kuendana na mfumo,”.

Boniface Pawasa

WACHEZAJI WAJENGWE KISAIKOLOJIA
Anasema ni wakati wa wachezaji kujengwa kisaikolojia kwani wanaonekana kutokuwa sawa na hasa ikizingatiwa wametoka kufanya vibaya katika mechi kadhaa zilizopita.

“Inatakiwa kuwajenga sana wachezaji kisaikolojia, wamepoteza mechi nyingi mfululizo, hawawezi kuwa sawa hasa wanapoona kwenye mitandao ya kijamii kuna watu wanalia, wanalalamika na wengine hata kupitez uhai,” alisema.

Beki huyo wa kati aliyestaafu kwa heshima alisema wachezaji wanatakiwa pia kujua Simba inahitaji nini, sio timu ya kusubiri matokeo ya mwisho ya kubahatisha.

“Imekuwa kero sasa watu wanasema Simba kikosi cha bilioni moja alafu kinafungwa na kikosi cha sh milioni taty, inaumiza sana, kwanza hakukuwa na haja ya viongozi kujitamba hivyo hadi sasa inakuwa shida, wajitathimini,”.

KUHUSU VIJANA

“Hata sisi tulivyofanya vizuri 2003 tulijiandaa, naona tunatakiwa tuwekeze kwenye soka la vijana kama tunavyowaona Azam FC wamepunguza gharama kubwa za kusajili wachezaji wa kigeni kutokana na vijana hao kuwasaidia.”

Alisema, anashangazwa sana na wachezaji wa kigeni wanaolipwa pesa nyingi halafu hakuna wanachokifanya, kitendo kinachowafanya wachezaji wengine kuvunjika moyo na kuoelekea kutiwajibika ipasavyo.

“Mbona Azam wanaendelea lufanya vizuri kupitia vijana wao, hivyo pia viongozi waongeze motisha mpira wa zamani ilikuwa ni wa kujitolea na kutembea kifua mbele, watoto wa siku hizi wanaona maisha ya akina Ronaldo, huwezi kuwadanganya lolote,”.

Msemaji wa Simba, Haji Manara akizungumza na Kichuya baada ya kufanyiwa mabadiliko

USHAURI KWA VIONGOZI

“Viongozi waondoe matabaka, nimeona Kichuya jana anatolewa anagoma alafu viongozi wanamfuata kumtuliza hii inaleta picha mbaya, Simba kulikuwa ana wachezaji wazuri kama akina Ulimboka ambao Kichuya hawafikii hata kidogo.”

Anasisitiza Simba ina viongozi ambao hawastahili kuwepo madarakani kwani waliojaa hapo ni wafanyabiashara tu, hata uchaguzi ukija uwezekano wa kushinda ni mkubwa tofauti na mtu kama yeye Pawasa ambaye anaujua mpira ila pesa kikwazo.

“Kwenye soka wamejaa wafanyabiashara, sisi watu wa soka tumewekwa kando kwavile hatuna pesa za kuwapa watu, hili ni tatizo kubwa sana.

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU KWA HABARI ZAIDI
Washirikishe rafiki zako habari hii kwa kuwatumia kupitia mitandao ya kijamii hapa chini

About Clezencia Tryphone

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *