Makala

Sio Mgosi tu, hata hawa walistaafu wakarudi tena uwanjani

on

LICHA ya majina makubwa kuhusika kwenye uhamisho wa dirisha dogo la usajili lililofungwa Disemba 23, 2017, kulikuwa na stori moja kubwa iliyomhusisha nyota wa zamani wa Simba na meneja mstaafu, Mussa Hassan ‘Mgosi’.

Straika huyo aliyewahi kupata mafanikio makubwa akiwa na wekundu hao alistaafu rasmi kucheza soka la ushindani Agosti 8, 2016 kwenye tamasha la Simba Day na kupewa kazi ya umeneja wa kikosi hicho.

Baada ya mwaka mmoja wa kuitumikia Simba kama meneja uongozi wa timu hiyo ulimbadilishia majukumu na kumpeleka kuwa kocha msaidizi wa kikosi cha vijana cha timu hiyo huku Dk. Cosmas Kapinga akivaa viatu vyake.

Taarifa za mkongwe huyo kusajiliwa kama mchezaji katika kikosi cha Dodoma FC kinachonolewa na kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ziliwashtua wengi huku baadhi wakishindwa kuamini lakini ukweli ukabaki kuwa hivyo na sasa Mgosi ni straika wa wakali hao wa mji mkuu.

Tayari Mgosi ameanza kuipatia mabao Dodoma FC na kuna kila dalili za kuisaidia timu hiyo kupanda ligi kuu. Lililotokea kwa Mgosi si jipya ulimwenguni, kuna nyota kadhaa walishawahi kustaafu na kurejea tena dimbani kwa sababu mbalimbali.

 

Jens Lehmann

Baada ya kuondoka Arsenal 2008, Lehmann alistaafu soka 2010 kabla ya kurejea tena mwaka mmoja baadae kufuatia makipa wote watatu wa Arsenal kupata majeraha.

Lehmann alipotezea tofauti zake za muda mrefu na Manuel Almunia na kukubali kusaini kama kipa wa akiba. Hata hivyo mkongwe huyo 42, alilazimika kuingia uwanjani katika mchezo dhidi ya Blackpool baada ya Almunia kuumia dakika chache kabla ya mchezo huo walioshinda mabao 3-1.

 

Johan Cruyff

Baada ya kustaafu kwa mara ya kwanza 1978, matatizo ya kiuchumi yalimlazimisha Cruyff kurejea uwanjani na kukipiga katika klabu ya Los Angeles Aztecs

“Nilipoteza pesa nyingi kwenye ufugaji wa nguruwe na hiyo ndio sababu pekee iliyonifanya niamue kurejea uwanjani ili kupata pesa ya kuendesha maisha,” alisema Cruyff wakati akirejea kucheza tena soka la ushindani kwa miaka sita, safari hiyo akitisha zaidi kwenye klabu za Ajax na Feyenoord alizowahi kuzitumikia ujanani.

Johan Cruyff

 

Robbie Rogers

Rogers aliamua kuachana na soka baada ya kutemwa na Leeds United akiwa na umri wa miaka 25 tu, baada ya hapo akaamua kujiingiza kwenye mapenzi ya jinsia moja.

Miezi michache baada ya kukiri kutojisikia vizuri kwa kitendo chake cha kustaafu soka, Rogers alijiunga na LA Galaxy na kuwa mchezaji wa kwanza anayefahamika wazi kuwa ni shoga kucheza ligi kuu za michezo yote. Sasa amestaafu moja kwa moja kutokana na majeraha ya mara kwa mara.

 

Stephen Carr

Baada ya kuachwa na Newcastle mwishoni mwa msimu wa 2008, Carr aliamua kutundika daluga kufuatia kukosa timu ya kucheza.

Hata hivyo Carr alirejea dimbani 2009 akiwa na kikosi cha Birmingham na kuwemo katika kumbukumbu ya ushindi wa kihistoria dhidi ya Arsenal yeye akiwa nahodha.

 

Roger Milla

Baada ya mcameroon huyu kustaafu 1989 na kuhamia katika visiwa vya Reunion vilivyo kwenye bahari ya Hindi, Rais wa nchi hiyo Paul Biya kipindi hicho alimuita na kumrejesha kwenye kikosi cha timu ya taifa kabla hajafanya maajabu nchini Italia 1990 kwenye kombe la Dunia akitupia mabao manne.

Baada ya kombe la dunia, Milla aliendelea kucheza soka na alipofikisha miaka 42 alikuwa mchezaji mkongwe zaidi kabla rekodi hiyo kuvunjwa na Faryd Mondragon 2014.

 

Carlos Roa

Roa aliamua kustaafu soka kutokana na imani za kidini wakati huo akiamini dunia ingefikia tamati 2000 hivyo kuigomea timu yake ya Mallorca kujadili mkataba mpya wakati uliokuwepo ukiwa unaelekea ukingoni.

Baada ya kuona dunia haijafika mwisho wa mzunguko wake na kwamba kila kitu kinaendelea kama ilivyokuwa 1999, Roa alirudi Mallorca na kumalizia mkataba wake.

 

Marc Overmars

Miaka minne baada ya kustaafu, Overmars aliziteka nyoyo za makocha wengi baada ya kuonyesha kiwango cha hali ya juu kwenye mechi ya kumuaga Jaap Stam, baada ya mechi hiyo alianza kupokea ofa mbalimbali.

Baada ya kipindi kirefu cha kukataa ofa hizo, mwisho aliamua kujiunga na timu yake ya kwanza ya Go Ahead Eagles ya Uholanzi.

 

Landon Donovan

Mfungaji bora wa muda wote wa ligi kuu nchini Marekani (MLS) alistaafu 2014 ila akaombwa kurejea 2016 kama mshauri ambapo tukio la wachezaji watatu wa kikosi cha kwanza kupata majeraha lilimlazimisha kuingia tena dimbani.

Hata hivyo nyota huyo hakufanikiwa tena kuipa taji timu yake ya LA Galaxy na akastaafu moja kwa moja mwishoni mwa msimu.

 

Tafadhali SUBSCRIBE kwenye BOIPLUS TV kwa kubofya picha hii hapa chini 👇

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU KWA HABARI ZAIDI
Washirikishe rafiki zako habari hii kwa kuwatumia kupitia mitandao ya kijamii hapa chini

About Karim Boimanda

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *