The sports Hub

A-Z: Simba Wanavyojiandaa Kumalizana na AS Vita Mapema

0 644

HABARI ya mjini kwa sasa ni harufu nzuri ya dalili za klabu ya Simba kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, utaongea nini kingine kisikike?. Bila kujali ni kwa wema au ubaya suala ni kwamba wadau wa soka kwa ujumla wanazungumzia suala hilo.

Simba wanakabiliwa na mchezo mgumu wa mwisho dhidi ya AS Vita Jumamosi hii kwenye dimba la Taifa ambapo matokeo pekee wanayohitaji ni ushindi. Bila shaka utakuwa umeelewa kwanini Msemaji wa timu hiyo Haji Manara alianzisha ‘slogan’ ya “DO or DIE”. Ni pointi tatu au mwisho wa safari umewadia.

Simba inapewa nafasi kubwa ya kuingia robo fainali si kwamba yenyewe ina kikosi bora zaidi ya vyote kwenye kundi lao bali ni kwavile imeutumia vema uwanja wake wa nyumbani tangu kuanza kwa michuano hii, pale kwa Mzee Mkapa wanasema ‘Hatoki Mtu’.

Maandalizi ya Wekundu hao safari hii yamegubikwa na mambo mengi ya kusisimua na ukiwatazama utajua kabisa kweli hii ni mechi ya mwisho na wapo tayari kwa lolote ilimradi tu ‘chama’ litinge robo fainali.

WACHEZAJI FULL MZUKA
Sijui wameahidiwa nini hawa jamaa, kila mmoja anaonekana ana ‘uchu’ wa kiwango cha juu na licha ya kuwa walibamizwa mabao 5-0 kule Kinshasa katika mchezo wa wao wa awali, huwezi kuona chembe ya hofu kwenye nyuso zao.

MAJERUHI WANAREJEA KWA KASI
Simba ilikuwa inakabiliwa na tatizo la majeruhi katika kikosi chao ambapo hadi sasa mchezaji pekee ambaye hafikiriwi kabisa katika mchezo huo ni Shomari Kapombe ambaye pia anaendelea vizuri.

Katika mazoezi ya jana, licha ya kupewa uangalizi maalum na madaktari, nyota Erasto Nyoni, Emmanuel Okwi na Pascal Wawa waliokuwa majeruhi walifanya mazoezi ya nguvu na wenzao kuashiria kuwa wanaandaliwa kwa ajili ya kipute hicho cha kukata na shoka.

MAKOCHA WAWAZUGA VITA KWA STORI KIBAO
Kama mashushu wa Vita walifika kwenye uwanja wa Taifa jana kwa lengo la kuwapeleleza Simba basi yawezekana hawakuambulia chochote kwani makocha wa timu hiyo walitumia muda mwingi kuzungumza na wachezaji kuliko kufundisha mbinu kwa vitendo.

Kikao kizito…..

Kocha mkuu Patrick Aussems na msaidizi wake Denis Kitambi walionekana wakizungumza na nahodha John Bocco kwa zaidi ya dakika 20 wakati huo wachezaji wenginge wakichezea mipira kama vile wanajiandaa na mechi dhidi ya timu ya ligi daraja la tatu.

Hata baada ya kuwaita wachezaji na kuwagawa bado makocha hao hawakuonekana kufundisha mbinu nyingi badala yake waliwaongoza wachezaji kufanyia mazoezi mambo ya kawaida tu.

HAO MASHABIKI SIJUI ITAKUAJE
Wakati wachezaji na makocha wao wakiendelea kuandaa ‘sumu’, huko mtaani na kwenye mitandao ya kijamii mzuka wa mashabiki hauelezeki kwa lugha rahisi. Ni kama vile mashabiki hao wanamuomba tu Mungu awafikishe salama siku hiyo ili wakaishuhudie timu yao pendwa ikiandika historia.

Wamesahau matokeo ya mchezo wao wa awali wamebaki na imani kuwa si jambo jepesi kuizuia Simba kupata matokeo chanya kwenye dimba la Taifa. Hii ni ishara kuwa kuna uwezekano mkubwa uwanja huo ukajaa Jumamosi hii.

Licha ya kiasi kikubwa cha pesa ambacho Simba watapata kutoka CAF, kuna faida nyingine kubwa kwa taifa ambayo ni kuongezeka kwa uwezekano wa kupewa nafasi ya timu zaidi katika michuano hiyo misimu ijayo kama Wekundu hao wataingia robo fainali na kuendelea vema.

Get real time updates directly on you device, subscribe now.