Kitaifa

Ally Mayayi Afunika Zoezi la Uchukuaji Fomu TFF

on

KIUNGO wa zamani wa timu ya Yanga Ally Mayayi amejitokeza kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya Urais wa Shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF) kwa mbwembe na shamrashamra akiongozana na wachezaji wa zamani wakiwa na mabango yenye ujumbe wa kumuunga mkono.

Katika wagombea wote tisa waliojitokeza kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo hakuna aliyeonekana kuungwa mkono na watu wengi kama ilivyokuwa kwa Mayayi kutokana na kusindikiziwa na wadau wengi wa soka wakati wa kuchukua fomu katika ofisi za TFF zilizopo Karume Dar es Salaam.

Kabla ya kuchukua fomu hiyo kulianza maandamano kutoka katika shule ya Sekondari Benjamin Mkapa hadi ofisi za TFF tukio ambalo lilivuta hisia za mashabiki wengi wa soka ambao wengi walionekana kuliunga mkono.

Akizungumza baada ya kuchukua fomu hiyo Mayayi alisema kwa sasa hatoongea chochote mpaka tarehe rasmi ya kampeni itakapotangazwa.

Kwa upande wake mchezaji na kocha wa zamani wa Simba aliyeinoa pia Mwadui FC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amewataka wachezaji wa zamani kumuunga mkono Mayayi hadharani kwani hata wasipojitokeza hawatakuwa salama kama uongozi uliopo utarejea madarakani.

“Hatupaswi kujifichaficha katika hili tunatakiwa kujitokeza kwa wingi wetu kumuunga mkono mwenzetu kwani akifanikiwa itakuwa rahisi kushughulikia matatizo yetu kwakua anayajua na ameyapitia ila tukimuacha peke yake hata sisi hatutaweza kuwa salama,” alisema Julio.

Nae nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania na Mtibwa Sugar ambaye nae alikuwa miongoni mwa waliojitokeza Salum Swedi alisema kwa sasa ni muda wa soka kuongozwa na wanasoka wenyewe ili kuleta maendeleo kwavile wanazijua changamoto zake.

“Huu ni muda muafaka kwa soka kuongozwa na wanasoka wenyewe na hili litafanikiwa kama tutakuwa na umoja kama tulivyoonyesha leo,” alisema mkongwe huyo.

Wengine waliochukua fomu leo katika nafasi ya Urais ni Shija Richard na John Kijumbe ambao wamefanya wagombea kufika tisa.

Mpaka sasa jumla ya wagombea 57 wamejiyokeza kuchukua fomu kwenye nafasi mbalimbali huku 47 wakiwa ni Wajumbe wa Kamati ya utendaji na watatu ni Makamu wa Rais.

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU KWA HABARI ZAIDI
Washirikishe rafiki zako habari hii kwa kuwatumia kupitia mitandao ya kijamii hapa chini

About Akram Msangi

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *