Kitaifa

AZAM: Tulieni, Kapombe Manula Hawaendi Kokote

on

UONGOZI wa klabu ya Azam umewatoa hofu wapenzi na mashabiki wao kuhusu nyota wao mlinda mlango Aishi Manula na mlinzi Shomari Kapombe kuwa wataendelea kuwa nao katika msimu mpya wa ligi licha ya kuwa na tetesi ya kutaka kutimka.

Katika wiki za karibuni baada ya kumalizika kwa ligi kuu ya Vodacom kumekuwa na tetesi mbalimbali kuhusu kutaka kutimka kwa baadhi ya wachezaji muhimu akiwemo Manula na Kapombe huku nahodha John Bocco ikisemekana amemalizana na mabingwa wapya wa FA timu ya Simba.

Msemaji wa klabu hiyo Jaffar Idd amewaambia waandishi wa habari kuwa nyota hao wapo kwenye hatua nzuri ya kusaini mikataba mipya baada ya ile ya awali kuelekea ukingoni na kinachosubiriwa ni wao kurejea kutoka kwenye majukumu ya timu ya Taifa.

“Manula na Kapombe tunaendelea kuwa nao katika msimu mpya mazungumzo yanaendelea vizuri tunasubiri warejee kutoka nchini Misri ili tumalizane nao. Niwatoe hofu tu kuwa hata wachezaji wenyewe wameonyesha nia ya kutaka kubaki nasi,” alisema Jaffar.

Msemaji wa Azam FC, Jaffar Idd

Jaffar alisema klabu hiyo imeachana na wachezaji Hamis Mcha na Ame Ally ‘Zungu’ baada ya kumaliza mikataba yao ambapo kwa sasa wapo huru kujiunga na timu yoyote wakiwa tayari wamepewa barua kufahamishwa jambo hilo.

“Wachezaji wetu Mcha ambaye tulikuwa nae kwa muda mrefu mkataba wake umeisha na hatutaendelea nae pamoja na Ame aliyekuwa Kagera Sugar kwa mkopo na tunawatakia maisha mema huko waendako katika safari yao ya mpira.”

Jaffar alithibitisha kuwa mkataba wa aliyekuwa Mtendaji mkuu wa klabu hiyo Saad Kawemba umemalizika na hawatoendelea nae badala yake Meneja mkuu Abdul Mohammed atafanya majukumu yote yaliyokuwa yakifanywa na kiongozi huyo huku cheo cha Mtendaji mkuu kikifutwa rasmi.

Kikosi cha Azam ambacho kimejipanga kutofanya matumizi makubwa ya fedha kwenye usajili kitaingia kambini Julai 3 kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi.

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU KWA HABARI ZAIDI
Washirikishe rafiki zako habari hii kwa kuwatumia kupitia mitandao ya kijamii hapa chini

About Boiplus Media

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *