Kitaifa

Azam Waanza Kuvuna ‘Shambani’ kwao

on

KLABU ya Azam FC imeanza kuona matunda ya kituo chake cha kulelea soka la vijana (Academy) baada ya kupandisha wachezaji watano kutoka timu ya vijana kuelekea msimu mpya wa ligi 2017/18.

Tayari uongozi wa klabu hiyo kupitia kwa msemaji wake Jaffar Idd umethibitisha kuwa hawatakuwa na nahodha wao John Bocco ‘Adebayor’ ambaye mkataba wake umemalizika huku taarifa zikiarifu kuwa amesaini miaka miwili na timu ya Simba hivyo kutoa nafasi kwa vijana hao kuleta changamoto mpya ndani ya kikosi cha ‘Wana lambalamba’ hao.

Meneja wa klabu hiyo Philip Arando ameuambia mtandao maalum wa timu hiyo kuwa kwa sasa Academy yao imeendelea kuimarika kwakua walikuwa wakitoa wachezaji wawili kila msimu lakini kocha mkuu Aristica Cioba amependekeza wachezaji watano ambao anataka kufanya nao kazi msimu ujao.

Arando amewataja nyota hao waliopandishwa kuwa ni mabeki wa kati Abbas Kapombe (aliyekuwa nahodha wa timu ya vijana), Godfrey Elias, Mohamed Omary, kiungo Stanslaus Ladislaus na mshambuliaji Yahaya Zaid.

“Azam imekuwa na utaratibu wa kupandisha angalau wachezaji wawili kila msimu kutoka timu ya vijana ila safari hii mwalimu (Cioba) amekuja na majina matano hali inayo onyesha Academy yetu inazidi kuwa bora,”alisema Arando.

Nyota hao wanafuata nyayo za wachezaji kama Aishi Manula, Metacha Mnata, Ismaili Gambo ‘Kussi’, Gadiel Michael, nahodha msaidizi Himid Mao ‘Ninja’, Mudathir Yahya, Abdallah Masoud na Shaaban Idd ambao walitoka kwenye Academy hiyo kabla ya kupandishwa na kuwa wachezaji nyota kwa sasa.

Wengine waliopandishwa ambao wako kwa mkopo ni kiungo mkabaji Bryson Raphael (Mbeya City) na Kelvin Friday (Mtibwa Sugar).

Timu hiyo ambayo kwa sasa ipo mapumziko baada ya kumalizika ligi itaanza mazoezi Julai 3 kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya mwezi Agosti.

Aidha Meneja huyo alisema kuwa kwa sasa wanaipitia ripoti ya kocha wao kwa ajili ya kufanya usajili ambapo kuna baadhi ya nyota kutoka nchini wamefanya nao mazungumzo lakini hakuwataja na kuwatoa hofu mashabiki wao kuwa wanaandaa timu bora ya ushindani msimu ujao.

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU KWA HABARI ZAIDI
Washirikishe rafiki zako habari hii kwa kuwatumia kupitia mitandao ya kijamii hapa chini

About Boiplus Media

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *