The sports Hub

Bila Mambo Haya Matatu Simba Yote ‘Ingehamia’ Wodini

1 725

DAKTARI Mkuu wa klabu ya Simba, Yassin Gembe amesema kitendo cha timu yao kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi na Klabu Bingwa Afrika kwa wakati mmoja ni mtihani mkubwa kwa afya za wachezaji wa timu hiyo lakini kuna mambo matatu yamesaidia kuokoa jahazi.

Akizungumza na BOIPLUS MEDIA muda mfupi kabla ya kuondoka Zanzibar jana kurejea jijini Dar es Salaam, Gembe alisema uwezekano wa wachezaji kuwa na uchovu uliopitiliza na hata kupata majeraha ni mkubwa kwavile walicheza mechi mfululizo huku wakikabiliwa na mechi kubwa na ngumu dhidi ya JS Saoura ya nchini Algeria.

“Hii hali inasababisha uchovu kwa wachezaji na uwezekano wa kupata majeraha pia ni mkubwa, kwahiyo tulichofanya sisi ni kuzingatia kanuni za kuurejesha mwili katika hali ya kawaida (recovery) kila tumalizapo mechi, bila hivyo hali ingekuwa mbaya, kwanza timu ingefanya vibaya na tungepata majeruhi wengi kila siku” alisema Gembe.

Daktari huyo alivitaja vitu ambavyo anahakikisha vinafanyika kila baada ya mechi kuwa ni kuwaingiza wachezaji kwenye maji yenye barafu, kuwashauri wanywe maji mengi pamoja na kuhakikisha wanapata muda mwingi wa kupumzika.

“Baada ya kila mechi ilikuwa ni lazima niwaweke kwenye barafu na wakitoka hapo nahakikisha wanakunywa maji mengi, haya ni mambo muhimu sana. Lakini pia yote hayo hayawezi kusaidia kama tu hawapati muda mwingi wa kupumzika.” Alisema Gembe.

Kuhusu suala la kupumzika Daktari huyo alisema mitandao ya kijamii imekuwa tatizo kwa wachezaji wengi kwani inawaweka ‘bize’ muda mwingi lakini kwa upande wa Simba anashukuru wachezaji wengi ni wazoefu na wanajitambua hivyo hatumii nguvu nyingi katika hilo, wanajiongoza wenyewe.

Simba itapambana na JS Saoura Januari 12 kwenye uwanja wa Taifa huku kikosi kingine kikiwa kimebakia mjini Unguja kwa ajili ya mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Malindi FC hapo kesho.

Get real time updates directly on you device, subscribe now.