The sports Hub

Chirwa Alitukosoa, Makambo Anatuzomea

0 700

OBREY Cholla Chirwa si jina geni kwenye masikio ya wapenda soka hapa nchini na pengine hata kwa wale wasioufatilia sana mchezo huo. Alisajiliwa kwa dau la sh. 200 milioni na klabu kongwe ya Yanga akitokea Zimbabwe alipokuwa akiichezea FC Platinum Star.

Chirwa alianza vibaya kazi yake ndani ya Yanga kwani hakuonesha cheche zozote kwenye mechi zake za awali jambo lililofanya kuzuka mijadala miongoni mwa mashabiki huku wengi wakihoji kiwango chake ukilinganisha na thamani ya pesa aliyosajiliwa.
Wengine waliamini kuwa usajili wa nyota huyo ulifanywa na wapiga dili wa mjini.

Kwangu ilikuwa tofauti, binafsi niliamini Chirwa ni mchezaji mzuri, tena ni karata dume kwa Yanga, kuanza kwake vibaya pengine kulitokana ugeni kwenye Ligi ya Bongo pamoja kubadili mazingira tu.

Chirwa akiwa na kocha Hans van Pluijm walipokuwa wakiitumikia Yanga, wawili hao sasa wapo Azam FC.

Maisha yalisonga huku Chirwa akiwa ni yule yule, habadiliki, alionekana ni kituko kila anaposhuka dimbani kuitumikia timu yake.

Baada ya safari ndefu iliyompitisha kwenye njia zenye mawe na miiba hatimaye Chirwa akaweza kufunga goli lake la kwanza kwenye Ligi Kuu katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar ndani ya dimba la Uhuru jijini Dar es salaam. Nini kilifuata baada ya pale? Chirwa alizidi kuimarika siku baada ya siku na kuwa mchezaji tegemeo kwenye safu ya ushambuliaji ya Yanga.

Wale waliokuwa wanamzomea na kumdhihaki sasa wakaanza kumpigia makofi na kumuona kama mfalme asiyevikwa taji kwao, hii ndo asili yetu watanzania, tuna ‘kaunafiki’ flani hivi mioyoni mwetu.

Labda nikupe mfano mdogo wa mchezaji Thiery Henry. Pengine atabaki kuwa miongoni mwa wachezaji bora kuwahi kuitumikia klabu ya Arsenal na atabaki kuwa miongoni mwa wachezaji wenye heshima kubwa kwa miamba hao wa jiji la London.

Kwanini nimetoa mfano wa Henry? ngoja nikueleze kidogo.
Wakati anasajiliwa 1999 akitokea klabu ya Juventus alikuwa ametoka kufunga magoli matatu tu kwenye mechi 16 alizoshuka dimbani kuitumikia timu yake hiyo.

Thiery Henry akiwa na Arsene Wenger

Mabosi wa Arsenal walikichukua kipaji kile wakiwa na imani mioyoni mwao kuwa ipo siku Henry atakuja kuwafanya watembee vifua mbele mithili ya mtu aliyepigwa ngumi ya mgongo.

Maisha yalianza kwenye klabu yake mpya ambapo hakuwa na mwanzo mzuri pale kwenye viunga Highbury akicheza zaidi ya mechi saba bila ya kufunga goli hata moja.

Viongozi na mashabiki walionesha uvumilivu kwa Henry, hawakumzomea, hawakumdhihaki, hawakumtusi wala kumpigia kelele. Najaribu kuwaza kwa sauti endapo Henry angekuwa huku kwetu, hakika angetamani hata kustaafu soka kama si kuihama timu yake.

Henry aliendelea na mapambano yake na taratibu akaanza kutikisa nyavu za timu pinzani. Mpaka sasa Henry anabaki kuwa mfungaji bora wa muda wote kwenye timu ya Arsenal, alifanikiwa kufunga magoli 174 kwenye mechi 254 alizoshuka dimbani. Naamini umeuelewa mfano wangu, turudi kwenye mada yetu sasa.

Chirwa…. baada ya ‘gari’ yake kuwaka.

Tumia dakika chache kuvuta kumbukumbu ya Chirwa alivyoanza maisha yake ya soka nchini Tanzania kisha linganishe na mshambuliaji wa sasa wa Yanga, Herithier Makambo.
Makambo alianza kupita kwenye barabara ile ile aliyopitia Chirwa, barabara yenye masimango, dhihaka, kejeli, dharau na matusi.

Kiwango chake kiliwafanya wengi waamini Makambo hastahili hata kuwa miongoni mwa wachezaji wa akiba kwenye klabu ya Yanga licha kufunga mara moja moja. Tatizo kubwa lililokuwa likilalamikiwa na mashabiki ni suala la kupoteza nafasi nyingi anazotengenezewa.

Japo tatizo hilo halijaisha moja kwa moja lakini ‘kiaina’ hii nchi imeanza kutulia. Unajua kwanini? kwa sababu Makambo ameanza kufanya yale ambayo wengi waliamini kuwa hawezi kuyafanya. Mpaka sasa amepachika mabao saba kwenye Ligi Kuu.

Heritier Makambo akimtoka beki wa KMC, Ally Ally katika mechi ya Ligi Kuu iliyozikutanisha timu hizo.

Zile kelele sasa hazipo tena, ndivyo tulivyo watanzania na hiyo ndio hulka yetu. Tunapenda mafanikio ya haraka, tunataka mchezaji akisajiliwa tu aanze kuonesha uwezo wake kwa 100% hata kama ikiwa ni kwenye mechi ya kwanza. Tunakosea, mpira haupo hivyo. Tusipobadilika basi tutaendelea kuwakosoa kwa maneno halafu wao wanatuzomea kwa vitendo uwanjani.

Tunapaswa kujua kuwa mpira wa miguu ni mchezo unaohitaji muda tofauti na uharaka tunaoutaka. Na hii si kwa wachezaji pekee, muda mwingine hata makocha wanaokuja kufanya kazi hapa nchini wamekuwa wakikumbwa na kadhia hii pale wanapoanza kwa kufanya vibaya.

Unakumbuka lile tukio lililomkuta kocha wa Simba Patrick Aussems jijini Mwanza? kama umesahau ngoja nikukumbushe kidogo. Baada ya Simba kupoteza mchezo dhidi ya Mbao pale CCM Kirumba kuna baadhi ya mashabiki walimzomea na kumpigia kelele kuwa hafai kuiongoza klabu hiyo, wengine wakithubutu hata kumrushia chupa za maji. Leo Simba inafanya vizuri, kumetulia na kupo shwari, hakuna hata shabiki anayenyanyua mdomo wake kumsema vibaya Aussems. Umeona asili yetu? sisi ndo watanzania bwana.

Imeandikwa na Swaleh Mawele
0657230793.

Get real time updates directly on you device, subscribe now.