The sports Hub

EDO KUMWEMBE: Historia Inatuhukumu, Acha Ujinga Uturudie

0 232

INASAMBAA video ambayo inamuonyesha Mrisho Ngassa akiwa amevunja mtego wa kuotea, mwamuzi msaidizi ananyanyua kibendera kuashiria ameotea. Majuzi ilikuwa inasambaa ya Mohamed Ibrahim, mwamuzi akamnyima bao.

Kiuhalisia wote hao hawakuwa wameotea. ‘Clip’ zao zimesambaa sana kwa sababu tu wanacheza Simba na Yanga lakini ukweli ni kwamba hata timu nyingine zinanyimwa mabao ya aina hii. Kwanini waamuzi wasaidizi wanakataa mabao haya?.

Kwanza kabisa na wao walikulia katika ujinga wetu kwamba mchezaji akikutwa na mpira akiwa peke yake basi hiyo ni ‘Offside’. Halafu kuna ile nyingine ambapo wachezaji watatu wanaweza kukutwa na mpira peke yao wakitazamana na kipa basi utasikia Ona ona, watatu wale Offside’.

Ngassa
Mrisho Ngassa

Ambacho hatujui ni kwamba kwa ‘movement’ ya mpira pamoja na uzembe wa mabeki, ni jambo linalowezekana kutokea wachezaji watatu wakatazamana na kipa na wote wasiwe wameotea. Tafuta bao la Nigeria dhidi ya Argentina Olimpiki 1996.

Ujinga huu umewabamba waamuzi wasaidizi na hilo husababishwa na mambo matatu. Kwanza wana hofu kwamba wasipoweka offside basi hawataeleweka kwa mashabiki kwa sababu mchezaji alibaki peke yake na kipa. Hawajiamini.

Pili, wanashindwa kusimama vema katika mstari mmoja na mchezaji wa mwisho, waamuzi wengi ni wazito na hawaendi na kasi ya mchezo. Lakini kubwa ni hii hofu ya kuruhusu bao ambalo mfungaji aliukuta mpira nyuma ya walinzi akiwa peke yake.

Sasa hivi tunawalaumu kwa sababu tuna Azam TV, shukrani kwa Azam. Lakini pia watanzania wameingia katika mchakato wa kwanza wa kujua Offside ni nini. Nadhani wanaachana na akili ya zamani kwamba mchezaji akibaki peke yake na kipa basi anakuwa ameotea.

Kitu kikubwa ni kwamba tukubaliane pale pale na maamuzi ya waamuzi pindi anaporuhusu bao ambalo mfungaji alijikuta amebaki peke yake na kipa. Tusitoe hukumu na kuwatukana, kuwarushia mawe na mengineyo mpaka tuone marudio kwanza. Wataondoa hofu na kuchukua maamuzi sahihi.

Kwa wakati ule wanahofia maisha yao kwa sababu wanajua tu kwamba hawataeleweka kwa kuruhusu bao ambalo mfungaji alikutwa na mpira peke yake akiwa anatazamana na kipa. Ni akili ambayo tulikuwa nayo tangu utotoni. Akili ambayo inatuadhibu kwa sasa. Imewaathiri waamuzi pia kisaikolojia.

 

Imeandikwa na mchambuzi wa soka nchini, Edo Kumwembe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram.

Get real time updates directly on you device, subscribe now.