The sports Hub

Hadi Sasa Yanga 11 Prisons 1, Ngoja Tuone Itakuaje

0 274

MPIRA wa miguu ni mchezo unaotajwa kuwa na matokeo katili zaidi huku pia ukisifiwa kwa tabia yake ya kutotabirika na kutojali historia na matokeo ya mechi zilizopita.

Mwenendo wa Prisons inayoikaribisha Yanga leo katika mchezo wa Ligi Kuu utakaopigwa kwenye dimba la Sokoine si wa kuridhisha hata kidogo ikiwa katika nafasi ya pili kutoka mkiani (19) baada ya kukusanya pointi 10 tu.

Yanga wenyewe wapo kileleni mwa msimamo wakiwa na pointi zao 35 lakini taarifa ya kutisha kwa Wajelajela hao ni kwamba Watoto wa Jangwani hawajapoteza hata mchezo mmoja msimu huu na kwamba wametoka kuchukua pointi sita kanda ya ziwa hivi karibuni.

Soka halitabiriki na hata mimi nisingependa kujiingiza katika mtego wa kuitabiria ushindi timu yoyote hapo lakini ukweli ni kwamba Yanga wapo vizuri zaidi kisaikolojia ukilinganisha na Prisons. Wajelajela wataingia uwanjani wakiwa na hofu ya kukutana na kinara tena asiyefungika.

Kikosi cha Prisons

Hadi sasa Yanga wameshinda mechi 11 wakati wenyeji wao hao wakiwa wameshinda mechi moja tu tena dhidi ya timu iliyopanda daraja msimu huu, Alliance FC. Ngoja tuone itakuaje leo.

Usiku wa kuamkia leo kuna mwiko umevunjwa katika Ligi Kuu nchini Ufaransa maarufu kama Ligue 1 pale Bordeaux walipoharibu rekodi ya PSG kwa kutoka nayo sare ya mabao mawili hiyo ikiwa ni baada ya mabingwa hao kushinda mechi zote 14 za kwanza za Ligi. Je, Prisons ndio watakuwa wa kwanza kuifunga Yanga? Nasema tena ngoja tuone itakuaje.

Silaha pekee ya Prisons ambayo ina udhaifu mkubwa kwenye safu ya ushambuliaji ni ukuta wake ambao bila kupepesa macho naweza kuutaja kama moja ya kuta imara zilizopo kwenye Ligi Kuu msimu huu ambapo hadi sasa umeruhusu mabao 11 tu katika mechi 14 walizocheza.

Licha ya kuwa katika nafasi mbaya kwenye Ligi, hadi sasa ni timu saba tu kati ya 19 ndizo zimefungwa mabao machache kuliko Prisons ambazo ni Azam FC (3), Simba SC (4), Yanga (7), KMC FC (7), Biashara United (9), JKT Tanzania (10), na Lipuli FC (10). Usiuchukulie poa huu ukuta ila ngoja tuone itakuaje.

Msimamo wa Ligi Kuu baada ya mechi za jana Disemba 2, 2018

Get real time updates directly on you device, subscribe now.