Habari za kuaminika za michezo na burudani kila wakati.

Hamumjui Lechantre Nyie, Nishusheni Nipande Gari yake Tafadhali

0 1,932

UKIWA hapa jijini Nakuru ndani ya daladala maarufu kama ‘Matatu’ ukasikia “Dere shukisha” basi ujue mtu ameshafika aendako ama ameahirisha kuendelea na safari hiyo. Kifuatacho hapo  ni dereva kuweka mguu ‘kati’ na kupaki gari.

Wakati mwingine mtu unaweza kumwambia dereva asimamishe gari ushuke baada ya kushtuka unakoelekea siko. Sio dhambi kushtuka mapema na kubadilisha mawazo. Tafadhali simamisheni gari lenu nipande la kocha Pierre Lechantre, nahisi litanifikisha niendako.

Kwasasa mtu anayeonekana tatizo zaidi ndani ya Simba ni Lechantre, yani hapa ni kuanzia kwa mashabiki, baadhi ya wachezaji na hata viongozi kadhaa, wameshindwa kabisa kumwelewa mfaransa huyo ambaye CV yake ni moto wa kuotea mbali.

Unajua kwanini hawa watu hawamwelewi Lechantre?, ni kwasababu tangu awasili hawaioni tena ile Simba ya kushambulia kwa kasi muda wote huku ikipiga pasi nyingi, Simba ya Lechantre ni inayozingatia zaidi nidhamu kwa kila timu huku ikilenga matokeo tu.

Hiki ndicho kilichomuondoa kocha Joseph Omog ambaye hadi anafungashiwa virago timu ilikuwa inaongoza ligi ikiwa haijapoteza mchezo wowote, watu wanataka burudani bwana, wakamleta Irambona Masoud Juma mtaalam wa 3-5-2 ambaye alizikonga nyoyo za Wanamsimbazi.

Lechantre anaonekana kama Omog mpya ndani ya Simba

Hata hivyo suala la uzoefu mdogo wa raia huyo wa Burundi kwenye michuano ya kimataifa liliwafanya vigogo wa Msimbazi wamlete Lechantre ambaye kwasasa wanahisi kama vile wamemrejesha Omog. Wengi tulishuka kwenye gari lake lakini leo nimebadili mawazo, narejea kwake kwa sababu zifuatazo;

 

NI KOCHA MKUBWA KULIKO INAVYODHANIWA

Kichwa cha yule mzee kina uwezo mkubwa sana wa kusoma mchezo, kwa kifupi Lechantre ni fundi wa mpira ambaye Simba ni kama wamebahatisha tu kumpata, si kocha wa kawaida na wanavyomchukulia ‘poa’ ni matusi kwake. Endapo raia wa Cameroon watasikia kejeli zenu watatamani kurusha ngumi, wao aliwapa ubingwa wa mataifa ya Afrika 2000 tena timu ikicheza mpira wa kiwango cha juu mno.

Majina ya timu alizofundisha ni alama nyingine ya ukubwa wa kocha huyo. Mbali na Cameroon, Lechantre amezifundisha timu za taifa za Qatar, Mali na Congo huku klabu kama Paris FC na Le Perreuex za Ufaransa pamoja na Al-Ahli, Club Africain, CS Sfaxien za Afrika zote zikiwa zimeshaonja ‘maufundi’ ya straika huyo wa zamani wa Monaco na Marseille.

Yawezekana Lechantre ni mkubwa mno kwa Simba ndio sababu bado wanashindwa kumwelewa. Niwakumbusheni tu Aprili 27, 2012 Senegal walimtangaza kama kocha mkuu wa timu yao ya taifa lakini wiki mbili baadaye alipiga chini mkataba huo kwavile walishindwa kutimiza matakwa yake.

HAJAANZA KUTUMIA MADINI YAKE

Lechantre ameikuta timu ikiwa katikati ya msimu na kikosi ambacho hakuhusika katika kukijenga lakini aliambiwa Simba ina ‘njaa’ ya ubingwa kwahiyo alichofanya yeye ni kuingiza gia ya kumalizia mlima. Hii ni gia namba moja ambayo kasi yake ndogo imesababisha watu waanze kumkataa, wamesahau kuwa hiyo ndiyo gia yenye nguvu kuliko zote.

Kwavile ana uwezo mkubwa na anajiamini ndio sababu aliziba masikio na kuliendea lengo lake bila kujali kelele za ‘Wajuaji’ wasiojua kitu ambao mwisho wa siku walishiriki kusherehekea ubingwa tena timu ikiwa haijapoteza mchezo wowote. Hii ni sifa ya kocha bora anayeamini katika mipango yake.

Ni wazi kuwa kocha huyo aliamua kutumia mipango ya muda mfupi ili tu timu ipate ubingwa halafu ndipo aanze kuingiza ‘sumu’ zilizowafanya Wacameroon wasimsahau hadi leo.

Niliwahi kumuuliza kwanini anaendelea kutumia mfumo ambao ni wazi hauwafurahishi baadhi ya viongozi, wachezaji na hata mashabiki wa timu hiyo?, jibu lake lilichangia kwa kiasi flani kuchochea maamuzi yangu ya kupanda ‘gari’ yake. Lechantre alisema ‘Huu si mfumo wangu, ni mfumo wa ubingwa kutokana na timu niliyoikuta, kama nisingefanya hivi nakuhakikishia tusingepata kombe msimu huu,”.

‘Babu’ huyo alinikumbusha mechi yao ya klabu bingwa Afrika dhidi ya Al-Masry iliyopigwa nchini Misri akisema alijaribu kufanya kile ambacho ataanza kukitumia baada ya kufanya marekebisho ya kikosi chake. Naamini mnakumbuka jinsi ambavyo waarabu walikuwa wakiomba mpira uishe, pale ndipo wengi tuliona upande wa pili wa Lechantre baada ya kuzuia kwa dakika 60 kisha baada ya hapo kushambulia kwa kasi ambayo hatukuwahi kuiona kwa miaka ya karibuni.

 

MWACHENI AWAONESHE ALICHOKUJANACHO

Kwa asilimia kubwa usajili unaoendelea sasa Simba ni mapendekezo ya kocha huyo na ukitazama kwa umakini utagundua ameanza na washambuliaji wenye kasi kama Marcel Kaheza na Adam Salamba, hii ni dalili ya maandalizi ya kile alichokifanya Misri ingawa kwa zogo linaloendelea mtaani sidhani kama ataendelea kuwepo kikosini hapo.

Lakini kwa akili ya mpira ilitakiwa apewe mkataba mpya ili iwe nafasi ya kuendeleza tabia yake ya kuheshimu kila timu lakini sasa akionyesha pia uwezo wake pale anapoamua kushambulia kwa 100% kitu ambacho msimu huu amekifanya katika mechi moja tu dhidi ya Al-Masry. Nimeamua kupanda gari yake ili kama ataongezewa mkataba basi na mimi nione alichokujanacho.

Mara kadhaa Simba imekuwa ikiacha makocha kutokana na presha za mashabiki lakini naamini kwa Lechantre hali inaweza kuwa tofauti, kama wataamua kumuacha aende zake basi sababu iwe ni gharama yake kubwa lakini kiufundi hakuna hoja ya msingi, kwasasa huyu ndiye kocha anayeweza kuwapeleka mbali kimataifa baada ya ujenzi wa kikosi kitakachoendana na falsafa yake.

 

Get real time updates directly on you device, subscribe now.

Comments
Loading...