The sports Hub

Machozi ya Mashabiki United na Kumbukumbu za Miaka ya 90

0 135

NANI haikumbuki ile Manchester United ya miaka ya 90? labda kwa wale tu waliozaliwa katika zama hizi za singeli ndio wasijua kwamba ilikuwa timu bora iliyowafanya makocha wengi wasitamani kukutana nayo, hakika ilikuwa ni tishio kwenye zama zile na kiufupi haikukamatika kirahisi.

Ilikuwa ni United iliyokusanya vipaji lukuki kutoka kwenye kila pembe ya dunia huku uwepo wa wachezaji kama Dwight Yorke, Andy Cole, Paul Scholes, Ryan Giggs, Erick Cantona na wengine wengi ukiwafanya watishe kwenye bara la Ulaya. Nani anabisha? anyooshe kidole juu ajifanye kama anajikuna.

Hakika ilikuwa timu ambayo kubeba mataji haikuwa stori kubwa kwao, yalikuwa ni maisha waliyoyazoea na kuwazoesha mashabiki wao ikicheza soka la kushambulia muda mwingi, haikuwa ajabu kwao kuondoka na ushindi mnono kila walipokutana na timu za kawaida.

United ilisifika barani Ulaya na duniani kwa ujumla kutokana na mtindo wao wa kutandaza soka safi lenye kuvutia jambo linalosababisha wengi watamani kurudi tena zama zile, zama ambazo mashabiki hawakuwa na hofu na timu yao wakitembea kifua mbele kwavile mataji yalikuwa hayakauki kabatini. Yes! hakika ile ndio Manchester United iliyobeba maana halisi ya neno ‘timu kubwa’.

Miongoni mwa vitu vinavyonifanya nijivunie kuishuhudia United ile ni yale maajabu waliyoyafanya Mei 26, 1999 katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya walipopambana na timu ya Bayern Munchen ‘The Bavarians’.

Ni dhahiri inaingia kwenye orodha ya fainali zilizobeba hisia za mashabiki kwa kiasi kikubwa kutokana na ubora wa timu zote mbili, imani yangu inanifanya niamini kuwa hakuna mtu aliyejuta kutazama fainali ile.

Upande wa Bayern, timu yao iliundwa na majemedari kama vlOliver Kahn, Matthaus, Babbel, Tarnat, Kuffour, Jeremies, Effernberg, Zicker, Jancker, Basler, Linker na wengine wakati United wenyewe wakijivunia nyota kama Peter Schmeichel (baba mzazi wa kipa wa Leicester City, Kasper Schmeichel), Garry Neville, Denis Erwin, Jaap Stam, Roony Johnsen, Nicky Butt, David Beckham, Ryan Giggs, Jesper Blomquist, Dwight Yorke, Andy Cole na wengineo. Hata hivyo Paul Scholes na Roy Keane waliukosa mchezo huo.

Katika dimba la Camp Nou mashabiki wapatao 90,245 waliushuhudia mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi wa kihistoria, Pierluigi Collina kutoka Italy, Bayern wakiwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Mario Basler lililofungwa kwa mkwaju wa adhabu ndogo.

Ferguson Alivyomaliza Ugumu wa Mechi kwa United
Kocha wa United Sir Alex Ferguson alifanya mabadiliko yaliyotengeneza historia kwa kumtoa Jesper Blomquist na kumuingiza Teddy Sheringham na baada ya dakika chache akamtoa Andy Cole na kumuingiza Ole Gunnar Solkjaer ambapo bao moja la Bayern liliendelea kudumu hadi ilipokuwa inaingia dakika ya 90.

Sheringham na Solkjaer hawakuhitaji dakika nyingi zaidi ya zile chache za nyongeza kuipa ubingwa United kwa kuifungia timu hiyo mabao mawili ya haraka yakiwaacha Bayern wakiduwaa wasiamini kilichotokea.

Najaribu kuiwaza United ile ya miaka ya 90 kisha nailinganisha na hii ya leo, United ya mabarobaro akina Jesse Lingard, Marcus Rashford, Chris Smalling na Ashley Young.

Akili yangu inanishawishi niamini kuna utofauti mkubwa sana wa viwango vya wachezaji wa zama zile na sasa, hii ya sasa ni United iliyojaza wachezaji wengi ambao hawajafikia ‘level’ za kutambua uzito na thamani halisi ya jezi ya timu hiyo. Wanaichukulia poa.

Wakati wengine wakiendelea kuamini kufeli kwa United kunatokana na falsafa za kocha Jose Mourinho, je vipi kuhusu David Moyes na Luis Van Gaal nao walishindwa kutokana na falsafa zao? hapana, akili yangu inagoma kukubali.

Pengine ni kweli kocha ana matatizo yake lakini United wenyewe wana matatizo zaidi.
Jaribu kutumia akili ya kiwango cha chekechea, kutoka zama za kumtegemea David Beckham, Andy Cole, Dwight Yorke, Eric Cantona,Teddy Sheringham, Ole Gunnar Solkjaer na Ryan Giggs. Leo hii ikamtegemee Jesse Lingard? hapana utakuwa ni utani, tena utani wa kuvutana mashati.

Itakuwa ni ajabu la karne kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya ukiwa na akina Marcus Rashford kwenye timu yako. Naomba nieleweke vizuri, siubezi uwezo wa Rashford au Jesse, ila bado hajakomaa kiasi cha kuweza kuibeba United mabegani mwake.

Wakati mwengine unatakiwa uitafute furaha hata kama itakugharimu kiasi gani, viongozi wa United ‘wawarudishe’ akina Rio Ferdinand kwenye kikosi, wamrudishe mpiganaji kama Paul Scholes, wamrudishe kiongozi shupavu kama Roy Keane, mashabiki wanatamani kumuona Jaap Stam mwengine.

Najua utanishangaa kwanini nimewataja hao, tulia, nielewe. Maana yangu ni hivi, viongozi wa Mashetani hao kwanza wajitathmini wao wenyewe kisha wawalete wachezaji wenye uwezo wa kupambania mataji, wachezaji wenye uwezo wa kuipigania timu na wenye hadhi ya kuvaa jezi ya Manchester United. Sina maana kuwa wachezaji wote waliopo pale ni dhaifu, hapana, hapana, narudia tena hapana. Wapo ila unaweza kuwahesabu kwa vidole.

Makala hii imeandikwa na mchambuzi chipukizi, Swaleh Mawele.

Simu: 0657230793

Get real time updates directly on you device, subscribe now.