The sports Hub

MAKALA: Mapinduzi Cup na Giza Lisilopata Mwanga

0 209

KATIKA ardhi ya Tanzania kuna matukio mengi ya kukumbukwa yamewahi kujitokeza na kuingia katika vitabu vya historia. Yapo yaliyofurahisha, kuhuzunisha, kustaajabisha au hata kukera.

Miongoni mwa matukio hayo ni lile la Januari 12, 1964 baada ya kutokea Mapinduzi ya Zanzibar.

Ni kumbukumbu itakayobaki katika vichwa vya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla vizazi hata vizazi.
Hii ilikuwa ni baada ya kuangushwa kwa utawala wa Sultan Jamshid bin Abdullah Al Said aliyeisimika mizizi yake ya utawala katika visiwa hivyo vya karafuu.

Katika kuienzi siku hii hasa katika upande wa mpira wa miguu, mamlaka ya soka visiwani Zanzibar ijulikanayo kama Zanzibar Football Association (ZFA) iliamua kuanzisha Kombe la Mapinduzi.

Ni mashindano ambayo mara nyingi hufanyika mwishoni mwa mwaka na kumalizikia mwanzoni mwa mwaka unaofuata japo mara chache huanza mwanzoni kama ilivyokuwa mwaka huu.
Baadhi ya timu kutoka Zanzibar, Tanzania bara na nchi jirani za Kenya na Uganda zimekuwa zikishiriki michuano hii.

Michuano hii ilianza rasmi kutimua vumbi mnamo 1998 ambapo timu ya Jamhuri ya Pemba ilifanikiwa kuwa ya kwanza kubeba ubingwa huo baada ya kushinda mabao 2-1 dhidi ya Shangani kutoka Pemba pia kwenye mchezo wa fainali.

Mwaka uliofuata haikuweza kufanyika badala yake ilifanyika 2001 na katika mwaka huo timu ya Polisi Zanzibar ikachukuwa ubingwa wake wa kwanza baada ya kuilaza Miembeni kutoka huko huko Zanzibar.

Timu nyingine zilizofanikiwa kubeba ubingwa wa michuano hii ni KMKM iliyochukua 2002, Yanga 2004, Mafunzo iliyobeba 2005.

Malindi pia ilichukua 2007, Miembeni ya Zanzibar 2008. Mtibwa Sugar ya Morogoro 2010, Simba SC ikabeba tena 2011 na Azam 2012.

Katika mwaka uliofuata (2013) Azam ilifanikiwa kutetea ubingwa wake na 2014 KCCA kutoka Uganda iliyoingia kama timu mwalikwa ikafanikiwa kuchukua taji hilo.
Simba ikachukua tena 2015. URA 2016, kisha Azam ikabeba mara mbili mfululizo 2017 na 2018

Licha ya ukongwe wa mashindano haya, mara zote yamekuwa yakikosa udhamini hali inayopelekea kuwa na mwenendo wa kusuasua mwaka baada ya mwaka hali inayopelekea mashindano kukosa mvuto unaostahili.

Inastua kidogo kuona waandaaji wa michuano hii ‘wamelala’ usingizi wa pono huku wakiyapeleka kimazoea zaidi.

Kama waandaaji wataamua kuyapandisha thamani mashindano ni itakuwa rahisi kuyafanya yawe na msisimko kuliko hata Kombe la Kagame.
Ndio! inawezekana, ni swala la maamuzi tu. Ni rahisi kuitumia historia ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuwavutia wawekezaji kisha wakawekeza pesa zao kwenye michuano hii.

Kama michuano hii ikipewa uzito wake na kuwekewa uwekezaji mkubwa na hatimaye kuwa miongoni mwa mashindano makubwa kwenye ukanda huu wa CECAFA itakuwa ni rahisi kuziona timu kubwa zinaomba mwaliko wa kushiriki na hapo itakuwa ni njia rahisi pia ya kuvitangaza vipaji tulivyonavyo.

Lakini hali imekuwa ni tofauti. Waandaaji hawaonekani kujaribu kuyapandisha thamani mashindano haya badala yake yanachukuliwa kama mashindano ambayo yapo kwa ajili ya kujifurahisha tu.

Imeandikwa na:
Swaleh Mawele
0657230793

Get real time updates directly on you device, subscribe now.