The sports Hub

Medali Yamchelewesha Kessy Kujiunga na Kambi ya Stars Sauzi

0 730

INAKARIBIA miezi minne tu tangu mlinzi wa kulia wa kimataifa wa Tanzania, Hassan Kessy ajiunge na Nkana Red Devils ya Zambia akitokea Yanga lakini tayari mambo yameanza kumwendea sawa kwa kupata mafanikio kadhaa klabuni hapo.

Licha kufanikiwa kupenya na kujihakikishia nafasi kwenye kikosi cha kwanza huku akitoa msaada mkubwa kwa timu, nyota huyo aliyewahi pia kung’ara na Mtibwa Sugar pamoja na Simba tayari ameifikisha timu yake fainali ya Kombe la Barclays inayopigwa Jumamosi hii kwenye dimba la Mashujaa wa Taifa lililopo Lusaka.

Katika fainali ya michuano hiyo yenye hadhi sawa na Kombe la Shirikisho la Azam Sports hapa nchini, Nkana watakipiga dhidi ya timu ya Ligi Daraja la kwanza ya Young Bufalloes mchezo utakaorushwa moja kwa moja katika chaneli ya Super Sport 9 (SS9) kwenye king’amuzi cha DSTV.

Kessy (mbele) akiitumikia timu yake ya Nkana Red Devils

Kessy ambaye amechelewa kujiunga na kambi ya timu ya taifa iliyopo Afrika Kusini akisubiri fainali hiyo ameiambia BOIPLUS kuwa anatamani watwae ubingwa huo ili aweze kuvaa medali yake ya kwanza klabuni hapo.

“Nitajiunga na kambi ya Stars baada ya fainali ya kesho (Jumamosi) ila kwasasa nipo Lusaka. Natamani tutwae ubingwa huu kwani litakuwa taji langu la kwanza hapa,” alisema Kessy.

Nkana ambao hawajawahi kutwaa kombe hilo toka lianzishwe, waliitoa Zesco katika hatua ya nusu fainali wakati Buffaloes wenyewe wakiitoa Green Buffaloes.

Get real time updates directly on you device, subscribe now.