The sports Hub

Mfupa wa Kibadeni Unaowatesa Wenye Meno Simba, Yanga

0 244

UNAPOZITAJA Simba na Yanga hakika unakuwa umezungumzia timu kubwa katika ardhi ya Tanzania na hata Afrika Mashariki kwa ujumla, mechi baina ya timu hizo ni mechi inayobeba hisia kali za mashabiki kila kona.

Mechi hiyo inayofahamika kama ‘Dar es Salaam Derby’ si tu huvutia mashabiki wa Tanzania bali hata wale wa kutoka sehemu mbalimbali ndani ya Afrika Mashariki kutokana na historia ya timu hizo pamoja na wachezaji wanaozitumikia.
Upinzani uliopo una asili mbili, kwanza ya kisiasa lakini pili ya kimpira.

Baada ya mchezo wa soka kuingia nchini kwenye miaka ya 1920 kisha ligi ya kwanza ya kimkoa kuanzishwa timu zilizoshiriki ligi hiyo zilikuwa za taasisi za Serikali au za raia wa kigeni.

Kulikuwa na timu ya jeshi ya Six Battalian King, timu ya wazungu ya Aga khan Club, Tanganyika Territorian, timu ya mamlaka ya reli iliyoitwa Tanganyika Railways, timu ya shule ya sekondari iliyoitwa Government School, Arab Sports, timu ya watu wenye asili ya Sudan “Sudanese Community” na timu ya wahindi ya Khalsan Club.

Baada ya mpira kuanza kupata umaarufu timu nyingi za wazawa zikaanza kujitokeza ili kushiriki ligi hiyo ambapo 1933 timu ya wazawa iliyoitwa New Young ikaanza kushiriki ligi hiyo ya mkoa. Ilipofika 1935 timu nyingine ya wazawa ikaanzishwa hii iliitwa Ilala Staff na ilianzishwa na wakazi wa Ilala.

New Young haikudumu kwenye ligi kwani mwaka huohuo ilishuka daraja kwa kile kilichorlezwa kwamba viongozi wa timu hiyo walikula pesa za michango na kuisahau timu hiyo. Jambo hilo liliwagawa wanachama wa timu hiyo na baadhi yao wakajitenga.

1939 baadhi ya wanachama waliojitenga wakaanzisha timu yao iliyoitwa Sunderland huku wanachama waliobaki kwenye timu ya New Young waliibadili jina timu yao na kuiita Young African (Yanga) wakati huo ligi ya mkoa ikisimamiwa na Chama cha Soka cha Mkoa kilichofahamika kama Dar es salaam Football Association.

Kikosi cha Sunderland cha 1966-1968

Aliyekuwa meya wa jiji kipindi hicho, Bwana Muhseen aliziunganisha Sunderland na timu ya waarabu (Arab Sports), huu ndio ulikuwua mwanzo wa ukaribu uliokuwepo baina ya Sunderland na watu wenye asili ya kiarabu.

Baada ya vita ya pili ya dunia mnamo 1938 timu nyingi za taasisi za serikali zikajitoa kwenye ligi hiyo. Hii ilipelekea kuchochea upinzani wa Sunderland na Young African kwa sababu zilibaki kama timu pekee kwenye ligi hiyo zilizokuwa na wafuasi wengi.

Mnamo 1942 timu ya Young African ilifanikiwa kuchukua ubingwa wa ligi ya mkoa.
Baada ya hapo utawala ukahamia kwa wapinzani wao (Sunderland) kwani walibeba ubingwa kwa mara nne mfululizo mpaka 1946.

1961 mpira wa miguu ukasambaa nchini na ilipofika 1965 ligi ya mkoa ilivunjwa na kuanzishwa Ligi ya Taifa.

1972 timu ya Sunderland ililazimika kubadili jina baada ya agizo la serikali kuwa timu zote ziache kutumia majina ya kigeni, hivyo ikaanza kuitwa Simba Sports Club.

Umaarufu wa Simba na Yanga umesababisha mechi yao kuwa ni kati ya Derby zenye msisimko mkubwa Afrika kama pale zinapokutana Al Alhy na Zamalek (Misri), Orlando Pirates na Kaizer Chiefs (Afrika Kusini) na Esperance na Es Setif (Tunisia).

Wachezaji wanaotumika kwenye mechi ya Simba na Yanga huwa kwenye presha kubwa kutokana na tambo za mashabiki wao inapokaribia mechi hiyo.

Inapotokea mchezaji akafanya vizuri katika mechi hii basi huo huwa ndio mwanzo wa kujijengea umaarufu mkubwa na atasifiwa kwenye kila kila kona au pembe ya nchi lakini endapo atafanya vibaya hali huwa tofauti na pengine ikawa ni sababu ya mchezaji kuondoka kwenye klabu hizi.

Abdallah Kibadeni

Wengi walifanya vizuri au vibaya katika mechi hizo na historia zao zikafutwa na matukio ya mechi zilizofuata lakini kuna jina la mtu mmoja ambalo ni kama vile liliandikwa kwa wino wa moto, huyu ni Abdallah Kibadeni aliyesajiliwa Simba 1970 akitokea Ilala ambapo kikosini hapo aliwakuta akina Arthur Mwambeta (marehemu), Haidary Abeid, Khalid Abeid, Athuman Mambosasa na wengineo.

Kibadeni anabaki kuwa mwanadamu pekee aliyewahi kufunga magoli matatu (hat-trick) katika mechi ya Simba na Yanga akitupia katika dakika za 10, 42 na 89 kwenye uliokuwa uwanja wa taifa (sasa Uhuru) Julai 19, 1972.

Mbali na wachezaji kama James Tungaraza, Iddi Moshi, Mark Sirengo na Emmanuel Okwi kujaribu kuifikia rekodi ya Kibadeni waliishindwa na kuishia kufunga magoli mawili pekee.

Siku zinakatika, miaka inasogea na bado ‘labda kesho, labda kesho’ zinaendelea. Je, nani ataweza kuutafuna mfupa huu wa Kibadeni?.

Imeandikwa na Swaleh Mawele
0657230793

Get real time updates directly on you device, subscribe now.