The sports Hub

Samatta Afunguka Kilichopelekea Asaini Mkataba Mpya Genk

0 691

BAADA ya taarifa kuzagaa kuwa nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Mbwana Samatta ameongeza mkataba katika klabu yake ya KRC Genk, mashabiki wengi wa straika huyo walionekana kutofurahia jambo hilo wakiamini litamchelewesha kusonga mbele zaidi ya Ligi Kuu nchini Ubelgiji.

Taarifa za Samatta kuongeza mkataba zilichukuliwa kama ni ‘ujanja’ wa Genk kuendelea kumzuia nyota huyo wa zamani wa TP Mazembe na Simba klabuni hapo lakini nyota huyo amefunguka kwamba mkataba mpya umesainiwa ukimbeba zaidi yeye kuliko Genk.

Akizungumza na BOIPLUS MEDIA mara baada ya kumaliza mchakato huo, Samatta alisema amelazimika kuongeza mwaka mmoja kutokana na sababu mbalimbali hasa zinazoihusu hatma ya soka lake barani Ulaya pamoja na kujenga mahusiano mema na Genk ili iwe rahisi kwa nyota wengine kutoka Tanzania kupita hapo.

“Mkataba ulikuwa unaisha 2020, nimeongeza mwaka mmoja hivyo sasa utaisha 2021. Kuna mambo kadhaa yamenifanya niongeze mkataba, siwezi kukutajia yote lakini suala la hatma yangu na taifa langu katika soka la kimataifa limezingatiwa zaidi. Hata hivyo uwezekano wa kupata timu nyingine Juni mwakani ni mkubwa.

“Mkataba wa awali haukuwa na kipengele kinachotaja thamani yangu kama timu itanihitaji, sasa kimewekwa, ni paundi 10 milioni, timu ipo kileleni mwa msimamo na mimi naongoza kwa magoli hivyo ilikuwa lazima nitulize akili uwanjani ili nione naweza kufanikiwa kati lipi kati ya ubingwa na ufungaji bora kwa lengo la kujiongezea thamani,” alisema Samatta.

Nyota huyo mwenye mabao 12 akiongoza orodha ya wafungaji kwenye Ligi Kuu, aliwahi kuiambia BOIPLUS kuwa hana tabia ya kukimbilia kuhama kabla hajaweka mizizi kwenye timu yake kwavile kwenye mpira kuna kufaulu na kufeli.

“Nawashauri hata wenzangu wasiwe wanakimbilia kuhama, huu mpira una mambo mengi, unatakiwa utoke sehemu wakati jina lako lina heshima kubwa ili hata huko uendako ukichemsha basi unarudi tu na unapokelewa kwa mikono miwili, maisha yanaendelea.

“Mfano, ningefeli Mazembe unadhani Simba wasingenirudisha?, ningerudi kwavile licha ya kucheza muda mfupi lakini tayari nilidhihirisha uwezo wangu pale, hata ningechemsha hapa Genk naamini Mazembe wangeniita haraka na ningepokelewa kwa mikono miwili. Kwahyo acha niweke alama yangu Genk halafu nitaondoka, muda si mrefu,” alimaliza Samatta.

Tangu ajiunge na Genk Januari 2016, Samatta amecheza mechi 141 akitupia mabao 55 na kusaidia upatikanaji wa mengine 14 huku kwa msimu huu pekee akiweka nyavuni mabao 21, kati ya hayo tisa kwenye Ligi ya Europa na 12 Ligi Kuu.

Klabu kadhaa barani Ulaya zimeonesha nia ya kumnunua straika huyo ambaye alianza kutangaza jina lake hapa nchini akiwa na African Lyon (zamani Mbagala Market) kabla ya kutua Simba.

Get real time updates directly on you device, subscribe now.