The sports Hub

Samatta Ana Furaha Lakini Bado Anaijutia Nafsi Yake

0 1,548

KAMA umewahi kukutwa na hali ya furaha na huzuni kwa wakati mmoja basi hakuna sababu ya kuelezewa sana juu ya kile anachojisikia Mbwana Samatta muda huu mara baada ya timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’ kuibamiza Cape Verde bao 1-0 na kufuzu fainali za mataifa ya Afrika mwakani nchini Cameroon.

Ishu iko hivi.….Boiplus Media ilimtafuta Samatta dakika chache kabla ya pambano hilo kumalizika lakini unajua kilichotokea, alipokea simu na kabla hajaambiwa chochote akasema “Naomba unipe dakika chache hivi ndipo unipigie tafadhali, siko vizuri. “

Wakati Samatta anazungumza hayo sauti ya mtangazaji wa Super Sport ilikuwa ikisikika akisimulia matukio katika mchezo huo ambao Uganda walikuwa wakihitaji ushindi au sare ya aina yoyote ili wafuzu. Hiyo ilitosha kumfanya mwandishi wa Boiplus afahamu kuwa nahodha huyo wa Stars alikuwa anafuatilia mchezo huo.

Patrick Kaddu aliifungia Uganda bao pekee katika mchezo huo

Ikawaje Baada ya ‘Game’ Kumalizika?
Kabla hata hajapigiwa simu, yeye mwenyewe alimtafuta mwandishi wetu na kwa bashasha ya hali ya juu akasema “Tangu nianze kucheza soka sijawahi kufurahia matokeo mazuri ya timu nyingine kama ambavyo nimefurahia ushindi wa Uganda leo, nimetazama mechi nikiwa na presha ya hali ya juu sana.”

Straika huyo wa KRC Genk ya Ubelgiji alitamka maneno hayo kufuatia ukweli kwamba kwa kitendo cha Uganda kuifunga Cape Verde basi Stars wanahitaji pointi tatu tu toka kwa Lesotho ili waweze kufuzu fainali hizo ambazo kizazi hiki cha sasa hakijui kabisa ‘ladha’ yake.

Kama Stars wataifunga Lesotho kesho Jumapili maana yake ni kwamba watakuwa wamefikisha pointi nane ambazo haziwezi kufikiwa na yeyote kati ya Lesotho na Cape Verde ambao watakutana katika mechi ya mwisho Machi mwakani.

Samatta akishangilia bao lake dhidi ya Cape Verde

Samatta Anajuta, Anajuta Sana
Licha ya kwamba asingeruhusiwa kucheza mechi ya kesho dhidi ya Lesotho kutokana na kuwa na kadi mbili za njano, kocha wa Stars Emmanuel Amunike alimjumuisha Samatta katika kikosi chake akiamini uwepo wake kambini kama nahodha na mchezaji mwenye uzoefu wa mechi za kimataifa, ungesaidia kwa kiasi kikubwa.

Hata hivyo Samatta alishindwa kujiunga na wenzake kambini nchini Afrika Kusini baada ya kuuguliwa na mtoto wake. Lakini yote tisa, kuna jambo linamfanya akose amani kabisa leo huku akijutia alichofanya Oktoba 16 kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam. Samatta anafunguka….

“Katika vitu ambavyo navijutia kwa sasa ni ile kadi ya njano niliyooneshwa katika mchezo wetu dhidi ya Cape Verde jijini Dar. Naijutia sana, natamani sana ningekuwepo Lesotho kucheza mechi ya kesho, natamani ningekuwepo nipigane na wenzangu kufanikisha azimio ambalo kila mtanzania mpenda michezo amekuwa akiliota. Lakini Mungu atajaalia na naamini wanajeshi wangu waliopo kule wataifanya kazi ipasavyo na tutafanikiwa In Shaa Allah!”

Samatta (katikati) akiwa na John Bocco (kulia) na Thomas Ulimwengu ambao wanatarajiwa kuongoza mashambulizi hiyo kesho.

Samatta alimaliza kwa kuwaomba wachezaji wenzake kufanya kila liwezekanalo ili kupata ushindi kesho huku pia akiwasihi watanzania kwa pamoja kuwaombea wanajeshi hao.

Stars itashuka kwenye dimba la Setsoto Jumapili hii katika mchezo huo mgumu unaoweza kuamua hatma ya Tanzania kwenye michuano hiyo. Mechi hiyo itaanza saa 11:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Get real time updates directly on you device, subscribe now.