The sports Hub

TABU IPO PALE PALE: Neymar, Mbappe Warejea Kuivaa Liverpool

0 60

INAONEKANA klabu ya PSG inaelekea kushinda vita ya kuhakikisha nyota wao Neymar na Kylian Mbappe wanakuwa ‘fit’ kuivaa Liverpool katika mechi ya kundi C ya Ligi ya Mabingwa Ulaya inayotarajiwa kupigwa kesho Jumatano, baada ya wawili hao kufanya mazoezi na wenzao jana Jumatatu, ESPN FC imepasha.

Nyota hao wa kimataifa wa Brazil na Ufaransa walishindwa kumaliza mechi za kirafiki za nchi zao Jumanne iliyopita baada ya kupata maumivu yaliyopelekea kuzuka kwa hofu kubwa klabuni kwao kuwa labda wangeweza kukosa mechi hiyo muhimu ya UCL.

Vyanzo vya karibu na miamba hiyo ya Ligue 1 vilipasha kuwa vipimo vya mwisho vilivyofanywa Ijumaa hii vilitoa majibu kuwa Neymar ana asilimia 50 ya kucheza mechi hiyo huku Mbappe yeye akionekana kuwa kamili.

“Nadhani Neymar na Kylian watakuwepo ingawa sina uhakika sana. Nina matumaini mengi kwavile walifanya mazoezi peke yao Jumamosi na naamini wataungana na wenzao Jumatatu,” alisema kocha Thomas Tuchel baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Toulouse Jumapili hii.

Neymar na Mbappe jukwaani

Baada ya wawili hao kumaliza salama mazoezi ya jana na wenzao ni kama vile sasa Tuchel ana uhakika atawatumia huku akikiri uwepo wao ni muhimu sana. Hata hivyo mjerumani huyo alisema kama atawakosa haitokuwa mara ya kwanza kucheza bila wao.

PSG wapo nafasi ya tatu katika kundi C baada ya mechi nne, pointi moja nyuma ya Napoli na Liverpool na moja zaidi ya Red Star Belgrade. Kwenye ligi ya Ufaransa wababe hao hawashikiki wakiwa pointi 15 juu ya anayewafuatia (Lyon) hiyo ikiwa ni baada ya kuibuka na ushindi katika mechi zake zote 14.

Wakati hao wa jiji la Paris wamebakiwa na kipindi kimoja cha mazoezi leo kuelekea mechi hiyo ya kukata na shoka hapo kesho na chanzo cha kuaminika kimesema Neymar na Mbappe watacheza mechi hiyo.

Get real time updates directly on you device, subscribe now.