The sports Hub

UEFA CL: Yaliyomo Katika Wiki ya Maamuzi Magumu

0 261

FUNGA mkanda, tulia kwenye kiti chako kwani tunaingia katika juma la maamuzi magumu kwenye Ligi ya Mabingwa barani Ulaya ambapo kuna timu zitakata tiketi ya kutinga hatua ya 16 bora, kuna zitakazokwenda kujiuliza katika Ligi ya Washindi barani Ulaya maarufu kama Uefa Europa League na baadhi zitaaga kabisa mashindano kwenda kusubiri msimu ujao wa 2019/20.

Kuanzia juma hili na yajayo, nahodha wako Mohammed Mshangama Jr. (VanMomo) nitaongozana nawe katika kuyachambua yale yote yatakayojiri katika majiji ya Manchester, Munich ,Roma hadi London. Tutapita Bate, St.petersburg, Amsterdam, Madrid, Paris, Turin na kutokezea Ankara na Brussels kabla hatujahitimisha safari yetu pale Estadio Wanda Metropolitano jijini Madrid Juni Mosi 2019.

AS ROMA vs REAL MADRID
Mchezo huu utapigwa katika dimba la Stadio Olimpico huku wenyeji AS Roma wakitarajia kutinga 16 bora kama tu watapata ushindi au sare mbele ya Los Blancos chini ya kocha Santiago Solari. Roma wanakumbuka kipigo cha magoli 3-0 walichokipata Santiago Bernabeu baada ya Isco, Bale na Mariano Diaz kucheka na nyavu.

 

Kwa upande wao Madrid kama wataibuka na ushindi katika mchezo huo watakuwa vinara wa kundi lao. Hata hivyo Madrid wanajivunia historia nzuri ya kutopoteza dhidi ya Roma kwenye UEFA kwa kuchukua pointi nne msimu wa 2001/02 na pointi zote sita 2004/05.

JUVENTUS vs VALENCIA
Machozi yaliyobubujika machoni mwake 2004 kwenye fainali ya Ulaya (Euro) kati ya Ureno na Ugiriki akishuhudia timu yake ya taifa ikikosa ubingwa, yalijirudia tena katika dimba la Mestalla pale alipoonyeshwa kadi nyekundu yenye utata safari hii akitoka dimbani na kuiacha Juventus yake ikiwa pungufu dhidi ya Valencia.

Ni Cristiano Ronaldo, baada ya kuitumikia Madrid kwa miaka tisa kabla ya kuhamia Turin anakutana na balaa hilo katika mchezo wake wa kwanza tu wa Ligi ya Mabingwa jambo ambalo lilipelekea aangue kilio kama mtoto aliyeachwa safari na mama yake. Ataingia katika mchezo huu wa marudiano akiwa na hisia kali na kumbukumbu za kilichotokea awali.

Sare tu katika mchezo huo itawapeleka Juventus raundi inayofuata huku pia wakiwa na nafasi ya kufuzu moja kwa moja hata wakipoteza kama tu Manchester United watafungwa na Young Boys pale katika jumba la sinema za ndoto za kutisha, Old Trafford.

Kama Valencia watapoteza mchezo huu na United wakashinda basi moja kwa moja Valencia watakuwa nje ya mashindano. Juventus itawakosa Alex Sandro na Emre Can huku Valencia ikiwakosa Gaya, Parejo pamoja na Soler.

#USISAHAU
Hadi sasa Ronaldo amecheza mechi 19 dhidi ya Valencia na amewafunga mabao 15.

MANCHESTER UNITED vs YOUNG BOYS
Kama nilivyoeleza hapo awali, Mashetani watapita kama Valencia watapoteza kule Turin ila utamu wa mechi ni kwamba ili Young Boys waende Europa basi wanatakiwa waifunge United, upo hapo?.

Msimu wa 2017/18 Jose Mourinho aliweza kuifunga timu kutoka Uswiss na kuwa kinara wa kundi lakini akatolewa na Sevilla baada ya kulazimishwa droo ya bila magoli nyumbani kisha kufungwa mabao 2-1 ugenini kwenye hatua ya 16 bora.

TOTTENHAM HOTSPUR vs INTER MILAN
Ili Spurs wajihakikishie nafasi ya pili kwenye B basi hawana cha kufanya zaidi ya kuibamiza Inter Milan kesho kwani kwa upande wao Inter wakipata ushindi tu wanakuwa wamejinyakulia tiketi moja ya kwenda 16 bora.

Inter itawakosa Brozovic, Perisic na Skriniar wanaotumikia adhabu ya kadi.

 

 

PSG vs LIVERPOOL
Hii ndio mbaya sasa, mbaya kabisa …..Parc des Princes jijini Paris ndipo kitakapopigwa kipute hicho. Huu ni mchezo wenye thamani kubwa kwa timu zote mbili. Mwili wa PSG utakuwa Paris lakini moyo na akili zitakua Stadio San Paolo kwenye mechi ya Napoli dhidi ya Red Star Belgrade.

Unajua imekaaje hii?
Napoli wakishinda watakuwa wamefikisha pointi tisa, sasa kama PSG watapoteza mchezo wao dhidi ya Liverpool kesho hali yao itakuwa mbaya kwani watabakiwa na pointi tano hivyo hata wakishinda mchezo wa mwisho itakuwa haijawasaidia kitu kwani watafikisha pointi nane huku Liverpool na Napoli wakiwa na tisa.

Hata hivyo, kurejea kwa Neymar na Mbappe katika kikosi cha PSG baada ya kupona majeraha yao yaweza kuwa habari njema kwa wanazi wa timu hiyo ambayo imecheza mechi 14 bila kupoteza hata moja katika Ligi Kuu nchini Ufaransa.

Neymar na Mbappe wakiwa mazoezini jana

#USISAHAU
Kocha wa PSG, ThomasTuchel ndiye alimrithi Klopp alipoondoka Borussia Dortmund.

#USISAHAU
Fabinho wa Liverpool na Mbappé wa PSG walikuwa kwenye kikosi kimoja cha Monaco kilichotwaa ubingwa wa Ufaransa 2016/17.

RATIBA KAMILI YA UEFA JUMA HILI:

Jumanne, Novemba 27
Group E: 
AEK Athens v Ajax
Bayern München v Benfica

Group F: 
Hoffenheim v Shakhtar
Lyon v Manchester City

Group G: 
CSKA Moskva v Viktoria Plzeň
Roma v Real Madrid

Group H: 
Manchester United v Young Boys
Juventus v Valencia

Jumatano 28 November
Group A: 
Atlético v Monaco
Dortmund v Club Brugge

Group B: 
PSV Eindhoven v Barcelona
Tottenham v Inter

Group C: 
Paris v Liverpool
Napoli v Crvena zvezda

Group D: 
Lokomotiv Moskva v Galatasaray
Porto v Schalke

Get real time updates directly on you device, subscribe now.