Makala

+VIDEO: Mafaili 10 ya Salum Kimenya

on

UKIANZA kuwataja mabeki makini wa pembeni katika Ligi Kuu ya Vodacom basi huwezi kuacha jina la beki wa kulia wa Prisons, Salum Kimenya.

Kimenya ambaye ni beki mwenye uwezo wa kukaba na kushambulia kwa kasi kubwa, amekuwa msumbufu kwa timu yoyote anayokutana nayo vikiwemo vigogo Simba na Yanga.

Kimenya huwezi kumkosa kwenye kikosi cha kwanza cha timu yake labda awe na matatizo kwani ana msaada mkubwa kwa Maafande hao wa Magereza kutokana na umakini wake, kujituma anapokuwa uwanjani.

Jopo la makocha ambao walichagua kikosi bora cha msimu uliopita hawakuweza kumwacha beki huyo kumuorodhesha kwenye kikosi chao, hiyo pekee imeonyesha ni jinsi gani Kimenya ni miongoni mwa wachezaji bora wachache kwenye ligi.

BOIPLUS ilifanya mahojiano maalumu na Kimenya ambapo alielezea mambo mbalimbali kuhusiana na soka lake, haya hapa ni mazungumzo yetu na Kimenya.

MSIMU ULIOPITA ULIMTOA JASHO
Kimenya anasema tangu aanze kucheza ligi kuu, msimu uliomalizika ndio ulikuwa mgumu sana kwake kwani ilikuwa ni ligi yenye ushindani mkubwa na matokeo hayakutabirika.

“Ukiangalia bingwa wa msimu ameamuliwa katika mechi ya mwisho, hata timu za kushuka daraja zilijulikana siku hiyo. Hiyo inatosha kueleza kuwa ligi ya msimu uliopita ilikuwa bora na ngumu kila mtu anaweza kuwa shahidi wa hilo,” alisema Kimenya.

BENCHI LA UFUNDI LILIWATOA KWENYE RAMANI


Beki huyo ambaye hajajumuishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ itayotarajiwa kupambana na Lesotho alisema baada ya kuondoka kocha Salum Mayanga timu yao iliyumba sana hali ambayo iliwapelekea hata kuwa miongoni mwa timu zilizokuwa kwenye hatari ya kushuka daraja.

“Kama unakumbuka msimu wa mwaka juzi kabla ya huu tulimaliza nafasi ya nne lakini kuondoka kwa kocha Mayanga timu ikayumba ila tunamshuru Mungu tumefanikiwa kubaki kwenye ligi.

“Mayanga anabaki kuwa kocha bora kwangu, ndiye aliyeifanya Prisons ikawa bora hadi tukafanikiwa kumaliza nafasi ya nne msimu wa 2015/16 hakuna kocha mwingine aliyefanya hivyo zaidi yake,”.

MBEYA ‘DERBY’ USIPIME
Kimenya anasema wanapokutana na majirani zao Mbeya City mchezo huwa mgumu kutokana na uhasama uliopo. Mchezo huanza kuchezwa nje ya uwanja ambapo mashabiki hujaa kwenye uwanja wa Sokoine. Mechi yao inakuwa haina tofauti kama zinapokutana Simba na Yanga za jijini Dar es Salaam.

“Prisons tupo tayari kufungwa na timu zote lakini siyo Mbeya City hata wao vivyo hivyo ni kama Simba na Yanga inavyokuwa,”.

BILA SH 50 MILIONI HUMVUI GWANDA


Mara kadhaa Simba imekuwa ikihitaji huduma ya beki huyo lakini wamekuwa wakishindwa kufika dau ambalo analitaka. Baada ya ligi kumalizika Singida United nayo ilitaka kumsajili ila bado tatizo likabaki kwenye maslahi.

“Nashindwa kujiunga na Simba tatizo ni moja dau lao dogo. Timu yoyote inayonihitaji nitakuwa tayari kuacha kazi yangu kwa dau la Sh 50 milioni na sio pungufu ya hapo,” alisema Kimenya.

CHIRWA, MSUVA, ABDUL ACHANA NAO

Simon Msuva

“Kiukweli Obrey Chirwa ni moja ya washambuliaji wenye kasi na anatumia nguvu zake vizuri huwa ninamhofia ingawa sio kwamba simuwezi. Ameleta changamoto kubwa kwenye ligi licha ya kupitia misukosuko mingi katika klabu yake, Simon Msuva naye yupo kwenye kiwango bora kwa msimu wa tatu mfululizo anastahili sifa.

“Kwa upande wa Juma Abdul ni beki bora wa kulia kwa sasa kutokana na uwezo wake wa kupandisha timu, kushambulia na kupiga krosi ambazo zimezalisha mabao mengi kwa Yanga. Licha ya kucheza mechi chache kama beki wa kulia, Juma alikuwa bora kuliko wengine msimu uliopita,”.

‘MAPROO’ NI SITA TU LIGI NZIMA WENGINE MMH!
Kimenya alisema wachezaji wengi wanaotoka nje ‘maproo’ wana viwango vya kawaida ambapo wengine wamezidiwa na wazawa ila viongozi wa klabu wanashindwa kuwapa thamani wanayostahili nyota wa ndani.

Kimenya amewataja Haruna Niyonzima, Donald Ngoma, Obrey Chirwa, James Kotei, Juuko Murshid na Yusuf Ndikumana kuwa ndiyo maproo wanaostahili kuendelea kuwepo kwenye ligi kuu ya Vodacom lakini wengine ni wa kawaida sana.

“Ukimtazama Niyonzima, Ngoma, Chirwa, Kotei, Juuko na Ndikumana unajifunza mambo mengi ni mafundi sana wa mpira ila hao wengine ni wa kawaida sana tumewazidi ila viongozi wanawapenda na kuwaamini japokuwa viwango vyao duni,”.

ELIMU NI TATIZO KWA WABONGO

Salum Kimenya kulia akiwa na mwandishi wa makala hii

Imeelezwa kuwa wachezaji wa Kibongo wengi wao huingia mikataba mibovu na klabu zao kwasababu hawana elimu ya kutosha ambapo mikataba mingine huwaletea shida. Kimenya anaelezea;

“Wachezaji wengi elimu zao ni darasa la saba, unacheza kwanza soka ndiyo ukasome na mkataba unaandikwa kwa lugha ya Kiingereza unafikiri kitu gani kitatokea hapo. Inabidi wapewe kwanza elimu kabla ya kusaini mikataba,”.

MNAOTAKA KUSAJILIWA SOMA HII
Kimenya amesema kipindi hiki ni kigumu na wachezaji wanapaswa kutuliza akili kabla ya kufanya maamuzi kwa mustakabali wa maisha yao kwani mpira ni ajira.

“Nawaomba wachezaji wenzangu kuwa makini sana kipindi hiki kwa kuchagua timu ambayo wanaona watapata nafasi ya kucheza tena waondoe ‘unazi’ wafanye mpira kama kazi kuna baadhi ya wachezaji wanasajili kwenye timu kwa ushabiki, hilo si jambo zuri mpira ni ajira na unatakiwa kucheza popote kikubwa ni maslahi na baada ya hapo ujitume kwa asilimia zote,”.

AKUMBUSHIA ISHU YA PAPE N’DAW WA SIMBA


Beki huyo anasema ushirikina upo sana katika soka la bongo ambapo baadhi ya wachezaji, viongozi na mashabiki wamekuwa wakijihusisha nao japokuwa kwa upande wake haijawahi kumtokea.

“Ushirikina ni imani, wapo wanaoamini ila mimi binafsi sina imani hizo. Nakumbuka mwaka juzi tulikuwa tunacheza na Simba yule mshambuliaji wao mrefu sana raia wa Senegal (Pape N’daw) alikuwa na hirizi kiunoni. Hiyo ni imani yake pia ingawa siamini kama mambo hayo yanasaidia,” alisema Kimenya.

KIKOSI CHAKE BORA CHA MSIMU WA 2016/17

1.Beno Kakolanya (Yanga),
2. Juma Abdul (Yanga)
3. Mohammed Hussein (Simba)
4. Nurdin Chona (Prisons)
5. Kelvin Yondani (Yanga)
6. Kenny Ally (Mbeya City)
7. Simon Msuva (Yanga)
8. Haruna Niyonzima (Yanga)
9. Mbaraka Yusuph (Kagera Sugar)
10. Obrey Chirwa (Yanga)
11. Ibrahim Ajib (Simba)

Kocha Meck Mexime (Kagera Sugar)

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU KWA HABARI ZAIDI
Washirikishe rafiki zako habari hii kwa kuwatumia kupitia mitandao ya kijamii hapa chini

About Boiplus Media

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *