Kitaifa

Viongozi wa matawi Simba wajibu mapigo ya wazee

on

VIONGOZI wa Matawi ya Simba wamepingana na kauli ya wazee wa Baraza la Udhamini chini ya Hamis Kilomoni wanaopinga mkutano mkuu wa wanachama kufanyika kwa madai ya wao kutokuwa na taarifa yoyote.

Kilomoni na wenzake jana waliweka wazi kuwa mkutano huo ni batili kwani viongozi halali waliopaswa kuitisha ni Rais Evans Aveva ambaye kwasasa anashikiliwa na vyombo vya dola kwa tuhuma za kughushi nyaraka na kutakatisha pesa.

Viongozi hao walisema kuwa mkutano huo uliotangazwa ndani ya siku 30 ni halali na muda wa kutaja ajenda ni siku saba kabla ya mkutano wenyewe kufanyika na muda huo bado haujafika.

Mwenyekiti wa matawi ya Simba, wilaya ya Temeke, Fortunatus Mwang’wela alisema kuwa viongozi walioteuliwa sasa kushika nafasi ya Aveva na makamu wake, Geoffrey Nyange bado wana nafasi ya kutoa ajenda za mkutano.

Mzee Hamis Kilomoni

“Mkutano upo pale pale kama ilivyopangwa, wanachama tujitokeze kwa wingi kama kuna mtu hataki mkutano ufanyike huyo anavunja katiba yetu kwani viongozi wamefuata taratibu,” alisema Mwang’wela.

Upande wa mwanachama mwingine, Albino Lwila alisema, “Hatufanyi malumbano ila tunapaswa kueleweshana mambo ya msingi yanayohusu klabu yetu, huu unakuwa kama utamaduni pale ambapo maendeleo yakitokea basi wengine wanaibuka kuyapinga.

“Mikutano yote miwili ya Agosti 13 na 20 ni halali kwa mujibu wa Katiba yetu, wanachama waje kwa wingi kujadili na kutoa maamuzi, alisema mwanachama huyo mwenye kadi namba 87.

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU KWA HABARI ZAIDI
Washirikishe rafiki zako habari hii kwa kuwatumia kupitia mitandao ya kijamii hapa chini

About Sheila Ally

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *