The sports Hub

ZAHERA: Nitamleta Mama Yangu Aje Kufunga Mabao Yanga

0 4,536

KOCHA wa mabingwa mara 27 wa Ligi Kuu Tanzania Yanga, Mwinyi Zahera ameonyesha kukerwa na ubutu wa safu yake ya ushambuliaji hadi kufikia hatua ya kusema atamleta mama yake awaonyeshe kazi akina Heritier Makambo.

Akizungumza mara baada ya mchezo dhidi ya Ndanda FC uliomalizika kwa sare ya bao moja, Zahera alisema wanatengeneza nafasi nyingi kila mechi lakini washambuliaji wake wanashindwa kufunga mabao.

“Kila mechi tunatengeneza nafasi, lakini kama washambuliaji hawafungi tutafanyaje?. Mfano nafasi aliyopoteza Makambo kwa kichwa, pale hata mama yangu angeweza kufunga,” alisema Zahera.

Heritier Makambo akijilaumu baada ya kukosa bao la wazi

Kocha huyo amekuwa akilalamika kuwa kikosi chake kinakosa wachezaji wengi wanaoendana na mfumo wake huku akitolea mfano nafasi ya mawinga ambapo ameweka wazi kuwa katika waliopo hakuna ambaye ameona anamfaa hadi sasa hivyo atasajili winga wakati wa dirisha dogo.

“Tunawabadilisha kila siku, Ngassa (Mrisho), Kaseke (Deus), Raphael (Daud) na leo mmemuona Jaffary (Mohammed) lakini hakuna anayeendana na mfumo wangu, mambo yakikaa sawa basi dirisha dogo nitatafuta mtu atakayefaa pale,” alimaliza Zahera.

Katika mchezo wa leo Ndanda ndio walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Nassor Hashim kabla Jaffary Mohammed hajaisawazishia Yanga.

Get real time updates directly on you device, subscribe now.